• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Hatimaye Miguna Miguna aonekana hadharani baada ya siku tano

Hatimaye Miguna Miguna aonekana hadharani baada ya siku tano

Bw Miguna Miguna alipofikishwa katika mahakama ya Kajiado Februari 6, 2018. Picha/ KANYIRI WAHITONa BENSON MATHEKA

HATIMAYE mwanasiasa Miguna Miguna alionekana hadharani kwa mara ya kwanza Jumanne, siku tano baada ya kukamatwa nyumbani kwake mtaani Runda Kaunti ya Nairobi.

Bw Miguna alionekana alipofikishwa katika mahakama ya Kajiado chini ya ulinzi mkali wakati kundi la mawakili wake walipokuwa mbele ya Jaji Luka Kimaru wa Mahakama Kuu ya Nairobi kufuatilia agizo alilotoa afikishwe mbele yake.

Mwanasiasa huyo ambaye ni wakili alionekana akizama kwenye mawazo alipokuwa akisubiri hakimu kuwasili kortini. Mawakili waliotumwa kumwakilisha walibishana na mkuu wa upelelezi katika kaunti ya Kajiado (DCIO), Bw Daniel Musangi, ambaye aliwazuia kuzungumza na Bw Miguna.  Hata hivyo, baadaye waliruhusiwa kuzungumza naye.

Bw Miguna alikataa kujibu mashtaka matatu ya kuhudhuria na kushuhudia “kiapo” ambacho kinara wa NASA Raila Odinga alikula Januari 30 katika bustani ya Uhuru Park, Nairobi.Shtaka la pili lilisema kwamba alihudhuria mkutano haramu bila kuarifu maafisa wa polisi jijini Nairobi na la tatu ni la kuwa mwanachama wa kundi haramu la National Resistance Movement (NRM).

“Sitajibu mashtaka yasiyo na maana. Huu ni ukiukaji wa haki zangu. Nimefungiwa kwa siku tano bila kuwasiliana na mawakili wangu na bila kuwasiliana na familia yangu. Nimeagizwa kufika mbele ya Mahakama jijini Nairobi,” alisema.
Wakili Koin Lompo alimwakilisha Bw Miguna.

Kulikuwa na mawakili wengine watatu na hakimu alipotaka kujua walikuwa wametumwa na nani Bw Miguna alizua kicheko kortini aliposema wote walikuwa wakimwakilisha. Koin alifahamisha mahakama kwamba Jaji Kimaru alikuwa ameagiza Bw Miguna afikishwe mbele yake na kwamba kumpeleka Kajiado kulikuwa ukiukaji wa haki zake. Kulingana na wakili Koin, hatua hiyo ilikuwa dharau kwa agizo la Jaji Kimaru.

Kwenye uamuzi aliotoka mwendo wa saa nane na nusu baada ya kukabidhiwa agizo la mahakama kuu, hakimu aliagiza Miguna kupelekwa mbele ya Jaji Kimaru kabla ya saa tisa alasiri kisha arejeshwe mbele yake kusomewa mashtaka Februari 14.

Alipokuwa akipelekwa seli, Bw Miguna alisikika akisema angali imara na hatishwi na mashtaka yanayomkabili.
Alipokuwa njiani kuelekea Nairobi, mawakili wake wakiongozwa na Dkt John Khaminwa walikuwa mbele ya Jaji Kimaru ambaye Ijumaa iliyopita aliamuru kuwa Miguna aachiliwe huru kwa dhama ya Sh50,000.

Alisema kuwa hangeondoka katika majengo ya mahakama hiyo hadi amri yake itakapotekelezwa. Jumanne asubuhi kundi la mawakili wanaomtetea Dkt Miguna walimuomba Jaji Kimaru asisite kuwasukuma jela Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Joseph Boinnet na Mkurugenzi wa Idara ya upelelezi wa jinai (DCI) George Kinoti kwa kukaidi na kudharau agizo la mahakama.

 

You can share this post!

Mahakama yaagiza polisi wasinase wakuu wa NASA

Wakenya wazua maswali kuhusu mawaziri wateule

adminleo