• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 8:55 AM
WANATAKAJE? Mzaha wao wa kung’atuka kisha kurejea ofisini wakosolewa

WANATAKAJE? Mzaha wao wa kung’atuka kisha kurejea ofisini wakosolewa

Na WAANDISHI WETU

TANGU makamishna wawili wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) warejee afisini ghafla, mnamo Ijumaa, miezi mitano baada ya kukwepa kazi, Wakenya wamekuwa na msururu wa maswali kuhusu lengo hasa la maafisa hao wakuu wa tume.

Aliyekuwa naibu mwenyekiti wa tume hiyo, Consolata Bucha Maina na aliyekuwa kamishna Margaret Wanjala Mwachanya, waliwashtua wafanyakazi wa tume akiwemo mwenyekiti wake, Wafula Chebukati waliporejea kimya kimya katika afisi zao jijini Nairobi licha ya kujiuzulu hadharani.

Miongoni mwa maswali ambayo Wakenya wanajiuliza ni kilichofanya makamishna hao kuamua kurudi katika tume inayoongozwa na Bw Chebukati waliyelaumu vikali wakidai alishindwa kuisimamia.

Wakati wa kujiuzulu kwao, walimtaja Bw Chebukati kama nahodha aliyeshindwa kudhibiti usukani na kuyumbisha shughuli za tume na kusema, hawangeendelea kuhudumu chini yake.

Japo walisema kwamba walichukua hatua ya kurejea kazini kufuatia uamuzi wa mahakama kwamba hawakufuata njia inayofaa kujiuzulu, Wakenya wanashangaa jinsi mtu anaweza kuwa na ujasiri wa kurejea kwa urahisi katika kazi aliyokwepa kwa miezi mitano baada ya kutangaza hakuitaka.

Jumapili, mashirika ya kijamii yalipinga vikali kurejea kwao kazini yakitaja hatua hiyo kama “mzaha mkuu.”

Mshirikishi Mkuu wa vuguvuvu la mashirika hayo, Suba Churchill, alisema watapinga kurejea kwa wawili hao kazini, kwa msingi kwamba, walijiuzulu hadharani, wakisema hawakuwa na imani na uongozi wa Bw Chebukati.

Naye mwanaharakati Okiya Omtatah alisema atafika kortini kuomba wazuiwe kurudi kazini akisema walikwepa kazi na kurejea kwao ni kitendo cha madharau. “Haiwezekani kuchukua tume kama nyumba ya kibinafsi kuingia na kutoka mtu anavyotaka,” alisema Bw Omtata.

Duru zinasema walipoondoka ofisini Ijumaa, Bw Chebukati aliagiza kubadilishwa kwa kufuli za ofisi zao, ili kuwazuia kuingia ndani. Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) pia inataka Bw Chebukati kufafanua kuhusu kurejea kwa makamishna hao ilhali bunge lilikuwa limeanza mchakato wa kujaza nafasi zao.

“Kweli, tumemwita Bw Chebukati, na wenzake walioko afisini, kutoa maelezo kuhusu masuala mengi katika IEBC ikiwemo kurejea kwa wenzao ambao walikuwa wamejiuzulu,” mwenyekiti wa kamati hiyo William Cheptumo akaambia “Taifa Leo” kwa njia ya simu.

Na ingawa Bw Chebukati aliagiza kubadilishwa kwa kufuli za ofisi zao, maswali yanaulizwa kuhusu walivyorejeshewa walinzi wao na lengo lao kurejea kazini baada ya kumkemea mwenyekiti huyo walipojiuzulu Aprili 6 mwaka huu.

Walipofika katika ofisi zao, Bw Chebukati na wafanyakazi wengine katika afisi hizo zilizoko jumba la Anniversary waliwapuuza. Kamishna wa tatu aliyejiulu Dkt Paul Kurgat, ambaye pia alijiuzulu hakuandamana nao lakini duru zilisema alipanga kurejea leo.

You can share this post!

Kijana maskini aliyekataliwa na mchumba aandaliwa harusi ya...

Polisi wamnasa mama wa kanisa aliyenyofoa nyeti za mumewe

adminleo