• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
KAULI YA WALIBORA: Dhima ya kutafsiri neno la Mungu haina masihara

KAULI YA WALIBORA: Dhima ya kutafsiri neno la Mungu haina masihara

Na PROF KEN WALIBORA

BIBLIA Takatifu ndicho kitabu kilichotafsiriwa kwa lugha nyingi zaidi duniani.

Mabilioni ya watu wanaosoma Biblia katika lugha zipatazo 2,600 kote duniani, wanafurahia tija ya tafsiri ya wengine. Hawa ni pamoja na wasemaji na wasomaji wa Kibukusu, Kimaragoli, Kinandi, Kikikuyu,na Kiswahili.

Biblia iliandikwa mwanzoni kwa Kiebrania na Kiaramu, hasa vitabu 39 vya kwanza na kitabu cha Mathayo.

Vitabu vingi vilivyoko katika ile sehemu iitwayo Agano Jipya, viliandikwa awali kwa Kigiriki.

Tafsiri ya kwanza kabisa ya Biblia ililenga kuvitafsiri vitabu vya Agano la Kale kutoka Kiebrania hadi kwa Kigiriki, shughuli iliyofanywa katika mji wa Aleksandaria, Misri kati ya karne ya 3 KK (Kabla Kristo) hadi karne ya 2 KK.

Wasemaji na wasomaji wa Biblia ya Kiswahili wamefaidi kwa miongo mingi tafsiri ya Union Version.

Hivi karibuni kuna matoleo mapya ya tafsiri ya Biblia katika Kiswahili kilichosasishwa.

Mathalani shirika la Biblica limejaribu kutafsiri Biblia kwa Kiswahili cha kisasa. Juhudi zilifanywa hadi kubadili majina kama Ibrahimu, Musa, Yusufu na Mariamu kusasishwa na kuwa Abrahamu, Mose, Yosefu na Maria.

Kwa nini Biblica wanaona haja ya kuyasasisha majina yaliyozoeleka katika Biblia? Yamkini msukumo mkubwa unatokana na wazo kwamba usuli au etimolojia ya majina haya ni katika Uarabu na Uislamu.

Kusasishwa kwayo kunaelekezwa na mwamko wao wa ‘kusafisha’ Uarabu na Uislamu katika Biblia ya Kikristo. Swali la kujiuliza ni kama hilo ni jambo mwafaka au linawezekana kutekelezwa kwa ufanisi.

Tukiamua kuyaondoa maneno ya usuli wa Kiarabu katika Biblia ya Kiswahili tutabaki na maneno mangapi? Yaani ni halali Kiswahili kukopa maneno kutoka kwa Kiingereza lakini Kiarabu haramu?

Maneno ya msingi kama vile “msamaha” “dhambi” na “dhabihu” yana asili ya Kiarabu. Alamin Mazrui amewahi kulizungumzia hili katika makala za kitaaluma, yaani juhudi za baadhi ya watafsiri wa Kiswahili kujaribu kuondoa kile wanachokiona kama Uarabu au Uislamu katika Biblia ya Kiswahili.

Je, nini hasa kinapaswa kupewa kipaumbele katika kusasisha tafsiri ya Biblia? Ni dhahiri kwamba Biblia ya Kiingereza imesasishwa ifaavyo kutoka kwa maneno kama vile Thou na Thee ya enzi ya William Shakespeare hadi kwa Kiingereza cha kisasi kinachoeleweka na wengi.

Kiswahili cha Biblia ya Union Version ambacho nacho kimewafaidi wasomaji wengi vilevile kimekuwa kikwazo kwa uelewaji.

Mathalani, nini kinachomaanishwa na “Yesu kuwa na maumbu zake” katika Kiswahili cha kisasa. Hilo neno halipatikani katika kamusi zilizowahi kuchapishwa wala yale yaitwayo makamusi. Mkilipata niambieni.

Ni baada ya utafiti mpana ndipo mtu anapobaini kumbe maumbo walikuwa ndugu na dada zake Yesu wengine ambao Mariamu/Maria aliwazaa. Umbu ni mmoja, na umbu wengi.

Jukumu la kutafsiri neno la Mungu ni zito. Watafsiri wanapaswa kuzika chukulizi zao.

Je, kati ya uelewaji na kusafisha Uislamu nini kinapaswa kupewa kipaumbele katika tafsiri ya Biblia ya Kiswahili?

You can share this post!

Yanga matumaini tele italima Rayon na Gor kutinga robo...

Huddah sasa akiri kuwezwa na uhodari kwa kidume kipya...

adminleo