• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:15 PM
TAHARIRI: Juhudi hizi nzuri za Uhuru zipigwe jeki

TAHARIRI: Juhudi hizi nzuri za Uhuru zipigwe jeki

NA MHARIRI

Wiki iliyopita, Wakenya walishuhudia ziara ya Rais Uhuru Kenyatta aliyeeelekea Marekani, ambapo alikutana na Rais Donald Trump.

Rais pia alikutana naye Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May ambaye alizuru nchini, na baada ya hapo anatarajiwa kuelekea China.

Ziara hizi zote zimekuja na ahadi fulani za miradi kwa taifa la Kenya, na matumaini ya wengi ni kuwa miradi na ahadi hizo zitapata kutekelezwa na kutimizwa.

Ni matumaini ya Wakenya wengi kuwa Kenya ikiendelea na ushirikiano wake na mataifa haya pia itanufaika na isiwe kuwa faida zinalalia upande mmoja.

Hata hivyo, katika harakati na juhudi hizi za rais, pia ni muhimu kuhakikisha kuwa Wakenya hawalimbikiziwi mzigo wa madeni. Ni kweli kuwa kuna hamu ya taifa hili kuinuka na kuimarika Zaidi, lakini hatua hizi zisiwe na za kumwekea mlipaji kodi mzigo mzito.

Ingawaje ni dhahiri kuwa deni la Kenya tayari ni mzigo mkubwa ndiposa kuna juhudi za kutafuta ushuru huku na huku kuona kuwa ulipaji wake hauwi changamoto kwa taifa, ni muhimu kwa taifa kutazama yale ya kuzingatiwa Zaidi.

Ni muhimu pia kuona kuwa hakuna mianya inasalia kwa watu wenye ubinafsi kutumia pesa zinazodhamiriwa kwa maendeleo na ustawi wa taifa, kuendeleza ufisadi.

Rais Uhuru Kenyatta anaendeleza vita hivi dhidi ya ufisadi, lakini kwa juhudi hizo kufaulu Zaidi, kuna umuhimu wa kuona kuwa hakuna pesa zinatengewa masuala ambayo yanatoa nafasi ya watu kuzifuja.

Hii ni sababu inashangaza kuona kuwa kila kukicha kuna wanaoshtakiwa kwa ufisadi na utumizi mbaya wa afisi zao, na kiasi cha pesa kinachohusika huwa cha kushangaza, hali ambayo inaibua maswali kuwa ni vipi kuna pesa nyingi ambazo zinatumiwa vibaya ilhali serikali inaendelea kukopa.

Lazima bajeti za wizara, mashirika na asasi husika za serikali ziweze kuandamwa vilivyo ili kuondoa mianya inayojitokeza hasa katika ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Lazima Wakenya waweze kujua jinsi fedha hizi zinavyotumika ili kuzuia ubadhirifu.

Kwa sasa, Wakenya wanahisi mzigo mzito wa gharama ya maisha na itakuwa vyema kwa watumishi wa umma waliopewa wajibu mbali mbali, kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uzalendo.

Lau sivyo, juhudi anazoendeleza rais Kenyatta kwa sasa zitakuwa bure. Lazima watu wakomeshe tamaa na kuishi kulingana na uwezo wao na sio kutamani makuu ama maisha ya juu ambayo yanawacha Kenya maskini Zaidi miaka Zaidi ya 50 tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Wakoloni.

You can share this post!

JAMVI: Mkakati mpya anaotumia Ruto kuhakikisha anatwaa...

JAMVI: Yatarajie haya Raila na Ruto wakimenyana debeni 2022

adminleo