• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
USAWA WA KIJINSIA: Shinikizo za utekelezaji wa Sheria ya Thuluthi Tatu zachacha

USAWA WA KIJINSIA: Shinikizo za utekelezaji wa Sheria ya Thuluthi Tatu zachacha

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) inaunga mkono shinikizo za wabunge wanawake za kutaka bunge lipitishe sheria inayosema kuwa uwakilishi wa jinsia moja bunge haupaswi kuzidi thuluthi mbili ya idadi ya wabunge wote.

Kwenye mahojiano na wanahabari katika jumba la Continental House, ambako mikutano ya kamati za huandaliwa, mwenyekiti wa kamati hiyo William Cheptumo alisema kamati iko tayari kuunga mkono mswada wa kufanisha azma hiyo.

“Inasikitisha kwamba ilivyo sasa bunge letu halijaafiki hitaji la katiba kuhusu usawa wa jinsia kwa sababu, idadi ya wabunge wanawake ni ndogo ikilinganishwa na wabunge wa kiume. Kwa hivyo, kamati yangu itafanya kila iwezalo kuhakikisha sheria hii ya thuluthi tatu imepitishwa… kwa sababu wajibu wetu ni kuhakikisha kuwa matakwa ya Katiba,” akasema.

Bw Cheptumo ambaye ni Mbunge wa Baringo Kaskazini alitoa wito kwa wabunge wanaume kuunga mkono msukumo wa wenzao wanawake wa kutaka sheria hiyo ipitishwe.

Kauli ya Bw Cheptumo inajiri siku chache baada ya wabunge wanawake kuzindua mbinu ya kipekee ya kuendeleza kampeni ya kutaka bunge lipitishe sheria hiyo ya usawa wa jinsia.

Mnamo Jumatano wiki jana zaidi ya wabunge 40 wanawake waliibua msisimko bungeni walipoingia kwenye ukumbi wa mijadala wakiwa wamevalia kichwani vitambaa vyeupe, hatua ambayo ilimshtua Spika wa Bunge Justin Muturi na wabungen wanauma.

Kiongozi wa wengi Aden Duale alimtaka Bw Muturi kutoa ufafanuzi ikiwa mavazi ya wabunge wanawake yaliafiki kanuni za bunge.

Mwenyekiti wa JLAC William Cheptumo akiongea katika jumba la Continental, Nairobi alipoahidi kuwa kamati yake itaunga mkono kupitishwa kwa sheria husu usawa wa kijinsia. Picha/ Charles Wasonga

“Nimehudumu katika bunge hili tangu mwaka wa 2003 lakini sijaona kila ambacho ninaona sasa. Je, mavazi haya ni sawa kwa mujibu wa sheria za bunge kuhusu mavazi. Mavazi haya yanaogofya. Hii ni imani fulani au itikadi ambayo haileweki,” akasema Bw Duale.

Naye Mbunge wa Lugari Ayub Savula aliwataka wabunge wanawake kuendeleza kampeni zao kwa njia zinazokubalika kwa mujibu wa sheria za bunge badala ya “kututisha kwa kuvalia mavazi ya kiajabu.”

Lakini Spika Muturi aliwatetea wabunge hao wa kike akisema walivalia sawasawa. “Wanaokana nadhifu. Mavazi yao ni nzuri na yanaafiki kanuni za bunge…. Tunapaswa kuwapongeza,” akasema.

Akiwahutubia wanahabari muda mfupi baada ya kuondoka nje, Mwenyekiti wa Kundi la Wabunge Wanawake (KEWOPA) Wangui Ngirici alisema wameamua kuwa watakuwa wakivalia vitambaa vyeupe kila Jumatano kila wiki hadi siku ambapo sheria kuhusu usawa wa kijinsia utapitishwa.

Mbunge huyo Kaunti ya Kirinyaga aliwataka Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kuwahimiza wabunge wanaume kupitisha sheria hiyo ambayo imeangushwa mara tatu katika bunge la kitaifa na mara moja katika Seneti.

“Kama wabunge waliochaguliwa na walioteuliwa tunashaangaa kuwa miaka minane imepita tangu katiba yetu izinduliwe lakini sheria kuhusu thuluthi mbili ya uwakilishi bungeni haijapitishwa. Leo (Jumatano) tumeanzisha kampeni ya kipekee kutetea kupitishwa kwa sheria hii,” akasema Ngirici.

Wabunge wanawake wakiwa wamevalia vitaa vyeupe muda mfupi baada ya kuondoka ndani ya ukumbi wa bunge. Mbunge Mwakilishi wa Migori Dkt Pamela Odhiambo anawaongoza wenzake kwa wimbo wa kushinikiza kupitishwa kwa sheria ya usawa wa jinsia, maarufu kama sheria ya thuluthi mbili. Picha/ Charles Wasonga

“Tutakuwa tukivalia vitambaa vyeupe kichwani kila Jumatano hadi sheria hii ipitishwe,” akaongeza Mbunge huyo wa chama cha Jubilee.

Mbunge Mwakilishi wa Kisumu Rosa Buyu ambaye ni naibu mwenyekiti wa KEWOPA naye alisema wanawake nchini wamevumilia kwa muda mrefu, akisema sheria hiyo inafaa kupitishwa mwaka huu bila kuchelewa.

“Wanawake wa Kenya waliipigia kura Katiba hii kwa matumaini kuwa iliwapa nafasi ya kuhakikisha kuwa wanawakilishwa ipasavyo katika asasi mbali mbali za uongozi. Lakini inasikitisha kuwa miaka minane baada ya kuzinduliwa kwa Katiba hii, sheria kuhusu uwakilishi wa wetu ndio ya kipekee ambayo haijapitishwa. Ama kwa hakika hii inatuvunja moyo zaidi,” akasema Bi Buyu ambaye ni Mbunge wa ODM.

Naye Naibu kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa Bi Cecily Mbarire alisema ikiwa sheria hiyo itapitishwa itasaidia pakubwa katika kusukuma masuala yenye umuhimu kwa sio tu kwa akina mama bali vijana na watu wanaoishi na ulemavu.

“Sheria hii itasaidia wanajamii wengi ambao hawajawakilishwa ipasavyo katika asasi muhimu za utawala nchini, muhimu zaidi ikiwa ni mabunge yote mawili. Kwa hivyo, tunawasihi wenzetu wanaume kuinga kampeni hii,” akasema Bi Mbarire.

Hata hivyo, Bw Cheptumo alitoa wito kwa wabunge wanawake kuhakikisha kuwa wanahudhuria vikao vya bunge wakati ambapo sheria hiyo itawalishwa bungeni baada ya bunge kurejelea vikao vyake mnamo Oktoba 2.

You can share this post!

Prof Kibwana tosha 2022, Wakenya mitandaoni waamua

Uhuru kona mbaya kutuliza ghadhabu za Wakenya

adminleo