• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Msaidizi wa gavana ndani kwa kuteka nyara mwanahabari wa NMG

Msaidizi wa gavana ndani kwa kuteka nyara mwanahabari wa NMG

Na JUSTUS OCHIENG

MAAFISA wa DCI Jumanne walimkamata Msaidizi wa Kibinafsi wa Gavana wa Kaunti ya Migori Okoth Obado, Michael Oyamo, kuhusiana na kutekwa nyara kwa mwanahabari Barack Oduor (pichani akiwa hospitalini) wa Nation Media Group.

Bw Oduor alitekwa nyara mnamo Jumatatu usiku katika hali tatanishi pamoja na Bi Sharon Otieno, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Rongo.

Jana, Mkuu wa Polisi wa Migori, Benedict Kigen alisema kuwa Bw Oyamo alikamatwa katika eneo la Uriri.

Mshukiwa alikamatwa muda mfupi baada ya Chama cha Kuwatetea Wanahabari (KUJ) na Baraza la Vyombo vya Habari (MCK) kukashifu tukio hilo huku vikiwataka polisi kuanza uchunguzi mara moja dhidi ya wahusika wakuu.

Vyama hivyo pia vilishinikiza hatua kali ya kisheria dhidi ya watakaopatikana kuhusika.

Wakati huo huo, Bw Obado alikanusha kufahamu lolote kuhusu kutekwa kwa mwanahabari huyo, ambaye anahudumu katika Kaunti ya Homa Bay.

Afisa wa Mawasiliano wa gavana huyo Nicholas Anyuor alitaja njama zozote za kumhusisha na kisa hicho kama mpango wa kumharibia sifa.

“Gavana Obado hafahamu lolote kuhusu mpango huo na jina lake halipaswi kuingizwa katika vitendo kama hivyo. Polisi wanafaa kufanya uchunguzi kamili ili kubaini wahusika wakuu,” akasema Bw Anyuor.

Bw Oduor na Bi Otieno walitekwa nyara muda mfupi baada ya kuondoka katika hoteli ya Graca eneo la Rongo. Bw Oduor aliruka kutoka gari hilo likiwa katika mwendo wa kasi katika Barabara Kuu ya Homa Bay-Kisumu na kupata majeraha. Kufikia jana jioni haikuwa imebainika aliko Bi Otieno.

Akizungumza na ‘Taifa Leo’, Bi Melida Auma, ambaye ni mamaye Atieno alibubujikwa na machozi.

“Sitaki kufikiria uwezekano wowote kwamba huenda wamemuua mwanangu. Nina imani kwamba yungali hai na kuwa hatimaye tutaonana,” akasema Bi Auma, ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi katika Kaunti ya Homa Bay. Aliongeza kwamba mwanawe ni mjamzito.

Idara ya Upelelezi (DCI) katika eneo la Nyanza ilisema kuwa shughuli za kumtafuta mwanafunzi huo zinaendelea. Mkuu wa idara hiyo katika eneo hilo Michael Baraz alisema kuwa uchunguzi wa kisa hicho utaharakishwa ili kubainisha ukweli kamili.

You can share this post!

Uhuru kona mbaya kutuliza ghadhabu za Wakenya

Ajiua sababu ya mke kuwa na mpango wa kando

adminleo