• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Shirika hili linaitaka korti iwarudishe kazini makamishna wa IEBC waliojiuzulu

Shirika hili linaitaka korti iwarudishe kazini makamishna wa IEBC waliojiuzulu

ABIUD OCHIENG na PETER MBURU

SHIRIKA moja la kutetea haki limefika kortini likitaka makamishna watatu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambao walikuwa wamejiuzulu waruhusiwe kurejea afisini.

Shirika la International Human Rights Defenders Care Well Society lilifika mbele ya Mahakama Kuu Jumanne, na kutaja hatua ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati kuwafungia nje makamishna Consolata Nkatha na Margaret Mwachanya waliporudi kazini siku chache zilizopita kuwa iliyokosa busara.

Bw Chebukati alisema mbeleni kuwa Bi Nkatha, Bi Mwachanya na Bw Paul Kurgat ambao walijiuzulu Aprili hawataruhusiwa kurudi kazini, akisema “IEBC haina afisi za waliokuwa makamishna.”

Alisema watatu hao walijiuzulu mbele ya umma n ahata kurejesha mali ya tume iliyokuwa mikononi mwao.

Shirika hilo sasa limesema kuwa kwa kufanya hivyo, Bw Chebukati alikiuka sheria kwani yeye sio mwajiri wao.

Mahakama Kuu wiki iliyopita ilisimamisha watatu hao kurejea kazini hadi kesi iliyofikishwa mbele yake na mwanaharakati Okiya Omtatah ambaye anataka makamishna hao wasiruhusiwe kurejea afisini isikizwe na kuamuliwa.

Bw Omtatah alieleza korti kuwa haja yake ni kulinda katiba na sheria ya nchi aliyosema “inatishiwa na vitendo vya watatu hao.”

“Kesi yangu ni ya kuzuia watatu hao kurejea kazini kwani wametangaza na kudhihirisha nia yao ya kurejea, baada ya kujiuzulu kwa hiari mnamo Aprili 16, 2018,” Bw Omtatah anasema kupitia karatasi za korti.

Anasema kuwa watatu hao waliapa kuwa wamejiuzulu kwa kumwandikia Rais na wakapokezana afisi zao.

Korti sasa itatoa maelekezo kuhusu kesi hiyo Septemba 17.

You can share this post!

KAULI YA WALIBORA: Shime kumuenzi nguli wa fasihi Prof...

Walimu wanaitisha wazazi Sh10,000 kuiba KCSE – KNEC

adminleo