• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Walimu wanaitisha wazazi Sh10,000 kuiba KCSE – KNEC

Walimu wanaitisha wazazi Sh10,000 kuiba KCSE – KNEC

OUMA WANZALA na PETER MBURU

BAADHI ya walimu watundu wamekuwa wakiitisha wazazi kulipia hadi Sh10,000 ili wanao waibiwe mtihani wa kitaifa wa mwaka huu, tume ya kitaifa ya kusimamia mitihani (KNEC) imetoboa.

Lakini tume hiyo sasa imewaonya wanafunzi na wazazi kuwa wanapewa ahadi butu kwani hakuna mtihani utakaoibiwa, akiwataka waliolipa pesa za aina hiyo kujua wameibiwa.

Waziri wa elimu Amina Mohamed aidha alisema kuwa kumekuwa na ushirikiano wa kuiba mitihani baina ya wazazi na walimu, akikashifu wanaofanya hivyo.

“Wanafunzi hawana uwezo wa kwenda kununua mitihani, ni wazazi na walimu wanaoendeleza tabia hii, lakini sasa tunataka wote wajue kuwa mtihani utakuwa sawa na hakuna atakayeiba,” akasema Bi Mohamed.

Ili kukomesha tabia hiyo, wizara imetoa adhabu kali kwa walimu, wanafunzi na shule zitakazopatikana zikijihusisha na visa vyovyote vya ukosefu wa uadilifu.

Katibu katika wizara hiyo Belio Kipsang alisema karatasi za majibu za wanafunzi watakaopatikana wakiiba hazitasahishwa, shule zitafutiliwa kutoka wizara na walimu watakaoendeleza watakamatwa na kushtakiwa.

Aidha, vituo vya mitihani vitapokea ulinzi was aa 24, huku wanafunzi wa shule za bweni wakikatazwa kutumia simu katika kipindi cha mitihani kwa sababu yoyote ile.

Mwaka uliopita, matokeo ya wanafunzi 1,205 katika mtihani wa KCSE yalifutiliwa baada ya kupatikana na makossa yanayohusiana na matumizi ya simu.

Bi Mohamed alisema vituo vya mitihani vitalindwa na polisi wenye sare na wapelelezi wasio na sare.

“Mitihani itafuata mkondo fulani uliotengwa kutoka makao ya KNEC hadi imfikie mwanafunzi,” akasema waziri huyo.

Jumla ya wanafunzi 1.7milioni watafanya mitihani ya kitaifa mwaka huu, 1,060,787 wakikalia KCPE na 663,811 wakifanya KCSE. Kutakuwa na vituo 10,075 vya mitihani kote nchini.

You can share this post!

Shirika hili linaitaka korti iwarudishe kazini makamishna...

Maiti ya mwanachuo mjamzito yapatikana msituni

adminleo