• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Wakenya waisifu #HarambeeStars kwa kuinyorosha Ghana licha ya kadi nyekundu

Wakenya waisifu #HarambeeStars kwa kuinyorosha Ghana licha ya kadi nyekundu

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA wamemiminia Harambee Stars pongezi baada ya timu hiyo kuwika nyumbani 1-0 dhidi ya Black Stars ya Ghana kwenye mechi ya Kundi F ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 uwanjani Kasarani, Jumamosi.

Huku nambari 45 duniani Ghana ikiomboleza kupoteza alama zote jijini Nairobi, nambari 112 duniani Kenya inasherehekea kupata ushindi wa kihistoria baada ya kufuzu matumaini ya kurejea AFCON kwa mara ya kwanza tangu ishiriki makala ya mwaka 2004 nchini Tunisia.

Baada ya mchuano huu wa kusisimua, ambao ulihudhuriwa na Kiongozi mashuhuri Raila Odinga na Waziri wa Michezo Rashid Echesa, Wakenya waliendeleza sherehe zilizoshuhudiwa na wachezaji uwanjani kipenga cha mwisho kilipolia kwa kujitosa kwenye mitandao ya kijamii.

“Vita vizuri na mchezo mtamu kutoka kwa timu iliyocheza wachezaji 10 na kuzaba Ghana 1-0 katika mechi ya kuingia AFCON mwaka 2019 uwanjani Kasarani, Nairobi. Ushindi huu unaweka Kenya pazuri kushindania tiketi. Hongera vijana wetu,” Naibu Rais William Ruto aliandika kwenye Twitter.

“Niliungana na Wakenya na mashabiki wa soka uwanjani Kasarani kwa mechi iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu na ghamu kati ya Harambee Stars na Ghana ambayo vijana wetu wameshinda 1-0. Leo ni siku ya wapenzi wa soka kujivunia kote Kenya,” Bwana Echesa aliandika kwenye Twitter.

Gavana wa Kaunti ya Nairobi Mike Sonko hakuachwa nyuma. “Pongezi timu yetu ya taifa ya soka Harambee Stars kwa kushinda Black Stars ya Ghana 1-0 katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019,” Sonko alichapisha kwenye mtandao wake wa Twitter.

Kocha Sebastien Migne hakuwa na huduma za kiungo nyota wa Tottenham Hotspur Victor Wanyama na beki matata David ‘Calabar’ Owino katika mechi hii.

Vijana wake wakiongozwa na mshambuliaji matata Michael Olunga walivuna alama tatu muhimu kupitia bao safi la kujifunga kutoka kwa beki Mghana Nicholas Opoku.

Olunga, ambaye alinunuliwa na klabu ya Kashiwa Reysol nchini Japan mwezi uliopita wa Agosti, alibana Opoku ndani ya kisanduku na kusababisha beki huyo kumwaga kipa wake Rchard Ofori dakika ya 40 baada ya krosi murwa kutoka kwa Eric Johanna.

Mchezaji Joash Onyango alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 61 na kulazimisha Kenya kusakata dakika zilizosalia wachezaji 10. Ghana ilijaribu kila mbinu kukomboa bao hilo bila mafanikio. Wanyama, ambaye amerejea kutoka mkekani baada ya kupona jeraha la goti, ameipongeza Harambee Stars. “Kazi nzuri Harambee Stars,” amesema.

Baada ya ushindi huu, Kundi F bado linaongozwa na Ghana kwa alama tatu. Ghana ilicharaza Ethiopia 5-0 katika mechi yake ya ufunguzi mwaka 2017. Sierra Leone ni ya pili kwa alama tatu ilizopata kwa kulipua Kenya 2-1 katika mechi ya kwanza mwaka 2017. Kenya inashikilia nafasi ya tatu kwa alama tatu kutokana na mechi mbili nayo Ethiopia inavuta mkia bila alama baada ya kusakata mechi moja na kuipoteza.

Kenya itsafiri Ethiopia hapo Oktoba 10 na kualika majirani hao jijini Nairobi siku nne baadaye katika mechi zake mbili zijazo za kufuzu kushiriki AFCON kabla ya kukaribisha Sierra Leone jijini Nairobi mwezi Novemba mwaka huu wa 2018. Itakamikamilisha mechi zake za makundi dhidi ya Black Stars nchini Ghana mwezi Machi mwaka 2019.

Historia ya matokeo ya soka kati ya Kenya na Ghana

Septemba 8, 2018: Kenya 1-0 Ghana (mchujo wa AFCON)

Machi 23, 2005: Kenya 2-2 Ghana (Mechi ya kirafiki)

Juni 13, 2003: Ghana 1-3 Kenya (Mechi ya kirafiki)

Septemba 18, 1996: Ghana 1-0 Kenya (Simba Cup)

Desemba 13, 1965: Kenya 3-3 Ghana (Mechi ya kirafiki)

Desemba 10, 1965: Kenya 2-13 Ghana (Mechi ya kirafiki)

Oktoba 21, 1964: Kenya 1-7 Ghana (Mechi ya kirafiki)

Septemba 30, 1964: Ghana 7-1 Kenya (Mechi ya kirafiki)

You can share this post!

Ratiba ya michuano ya ligi ya Super 8

Mke ajigeuza umbo baada ya kunyofoa nyeti za mumewe

adminleo