• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Wandani wa Sharon wapokea vitisho

Wandani wa Sharon wapokea vitisho

Na RUTH MBULA

WATU ambao walikutana na Sharon Otieno kabla ya kukumbana na mauti yake wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana.

Vile vile, wale ambao walitangamana na mwanahabari Barack Oduor Nation Media Group wamekuwa wakiishi kwa hofu kutokana na vitisho sawa na hivyo.

Familia ya Bi Otieno pia imekuwa ikipokea vitisho, hata inapoomboleza kifo cha mwana wao.

Vitisho hivyo vinatoka kwa watu wanaowapigia simu kwa namba zilizofichika.

Wale ambao wamepokea vitisho hivyo washaandikisha taarifa kwa polisi.

Wachunguzi wanafuatilia watu ambao wanatekeleza vitisho hivyo wakilenga kubaini asili yao na ikiwa ndio walihusika katika mauaji ya Sharon.

Mjomba wa marehemu, ambaye hakutaka kutajwa kwa sababu za kiusalama, alisema jana kwamba baadhi ya marafiki na jamaa zao, wamekuwa wakiwaomba “kulegeza kamba katika kufuatilia kiini cha kifo cha Sharon.”

Alisema kuwa anaamini kuwa huenda jamaa hao wana uhusiano na wale ambao walihusika katika mauaji ya binti yao.

“Baadhi ya marafiki wetu, jamaa na hata waombolezaji wamekuwa wakituomba kutozungumzia sana suala la Sharon. Ijapokuwa wanajifanya wanaomboleza nasi, nadhani kuna njama wanapanga,” akasema.

Hata hivyo, alisema kwamba hatatishika hata kidogo, ila ataendelea kushinikiza haki kwa mpwawe, aliyekuwa akisomea masuala ya uwekaji rekodi za matibabu. Kufikia kifo chake, Sharon alikuwa na mimba ya miezi saba.

Mnamo Ijumaa, msemaji wa familia hiyo Joshua Okong’o aliwatahadharisha wanasiasa na vyombo vya habari dhidi ya kueneza uongo kuhusu kifo chake.

Akizungumza na wanahabari nyumbani kwa marehemu, katika kijiji cha Magare, Kaunti ya Homa Bay, Bw Okong’o aliwaomba wanasiasa kutolizungumzia suala hilo ili kuwapa wachunguzi nafasi ya kubaini kilichofanyika.

Alieleza kuwa kutiwa chumvi kwa tukio hilo kulipelekea kifo cha shangaziye Sharon, Deborah Ogweno, ambaye alizimia na kufariki mnamo Ijumaa. Alikuwa na umri wa miaka 44.

“Alizimia wakati aliposikia vyombo vya habari vikiripoti semi za wanasiasa kuhusu kifo cha Sharon,” akasema.

You can share this post!

MAUAJI YA SHARON: DPP tayari kunasa Gavana Obado

Maandalizi ya mitihani ya KCPE na KCSE yako tayari –...

adminleo