• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:21 AM
Ufisadi ndio kiini cha njaa Afrika – Wataalamu

Ufisadi ndio kiini cha njaa Afrika – Wataalamu

Na LEONARD ONYANGO akiwa Kigali, Rwanda

UFISADI unachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa baa la njaa nchini Kenya pamoja na mataifa mengineyo ya Afrika.

Kulingana na wataalamu na viongozi wa mashirika mbalimbali ya kimataifa, ufisadi unasababisha njaa barani Afrika sawa na mabadiliko ya hali ya hewa na viwavi vinavyoharibu mazao.

Wataalamu hao wanaamini kuwa siasa mbovu na ufujaji wa fedha za umma vitazuia bara la Afrika kuwa na chakula cha kutosheleza raia wake kufikia 2030.

Akizungumza katika kongamano kuhusu kilimo la 2018 lililokamilika wikendi jijini Kigali, Rwanda, aliyekuwa naibu waziri wa mashauri ya kigani wa Amerika Jendayi Frazer alisema ufisadi katika sekta ya kilimo na uchoyo wa wanasiasa vimeathiri pakubwa uzalishaji wa chakula cha kutosha barani Afrika.

Dkt Frazer, ambaye pia ni mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalosaidia wakulima wa mashamba madogo kupata masoko ya bidhaa zao, Africa Exchange Holdings, alisema uwazi unahitajika katika sekta ya kilimo ili kuwezesha bara la Afrika kujikomboa kutokana na makali ya njaa.

“Kiongozi anachaguliwa leo na kesho anaanza kukusanya fedha atakazotumia katika uchguzi ujao. Miradi michache wanayotekeleza inalenga kuleta kura na wala si kuwainua watu kiuchumi. Bila kuwepo na uadilifu katika sekta ya kilimo njaa itaendelea kuwa donda ndugu barani Afrika,” akasema Dkt Frazer.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair alisema ukosefu wa sera na uadilifu ni pigo kwa uzalishaji wa chakula.

“Inasikitisha kwamba mamilioni ya watu barani Afrika wanaendelea kukosa chakula ilhali ardhi imejaa rutuba,” akasema Bw Blair ambaye pia ni mwenyekiti wa taasisi ya Tony Blair Institute for Global Change.

Naye Rais wa Wakfu wa Rockefeller, Rajiv Shah alisema ufisadi huenda ukatatiza ndoto ya Afrika kuwa na chakula cha kutosha kufikia 2030.

“Ni kweli kwamba ufisadi umekita mizizi katika sekta ya kilimo na unahitaji viongozi wakakamavu kukabiliana na janga hilo,” akasema Dkt Shah.

Rais wa Shirika la Kimataifa la Ufadhili wa Ustawi wa Kilimo (IFAD) Gilbert Houngbo alisema ni kiasi kidogo mno cha fedha zinazokusanywa na serikali kutoka kwa wahisani zinawafikia wakulima wa mashamba madogo, ambao huzalisha asilimia 80 ya chakula kinachotumiwa barani Afrika.

Ripoti ya mwaka huu kuhusu Hali ya Kilimo Barani Afrika inaonyesha kuwa maafisa serikalini hupenda kuwekeza katika miradi mikubwa ili kupata mgao wao wa ufisadi na kutelekeza wakulima wadogo.

Nchini Kenya, ufisadi umekithiri katika kila hatua ya uzalishaji katika sekta ya kilimo.

Wakulima wanakabiliwa na uhaba wa mbolea ambapo wengi wao wanauziwa feki.

Kadhalika kuingizwa kwa bidhaa za magendo humu nchini pia kumeathiri wakulima kwani mazao yao hukosa soko.

You can share this post!

Ogiek waapa kuunga mkono uhifadhi wa msitu wa Mau

Kibaki amsifu marehemu Godia kama mwanamageuzi

adminleo