• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
UTAMADUNI: Ngombe 14 wanatosha kufidia kifo cha mwana – Familia

UTAMADUNI: Ngombe 14 wanatosha kufidia kifo cha mwana – Familia

Na PIUS MAUNDU

FAMILIA ya mwanaume aliyeuwawa kutokana na mzozo wa Sh50 katika katika Kaunti ya Makueni, imekubali kupokea ng’ombe 14 kama fidia kutoka kwa ukoo wa mshukiwa wa mauaji.

Hatua hiyo ya familia ya Sila Mutua, mshonaji viatu, ambaye alikumbana na kifo chake Jumapili moja mnamo Juni, imewashangaza wengi wasiofahamu tamaduni ya ‘Maambo’ iliyotumika tangu jadi kusuluhisha kesi mbalimbali katika jamii ya Akamba.

Jamaa za mwendazake aliyefariki baada ya kipigo kikali kutoka kwa mteja wake hata hivyo wamelazimika kusubiri zaidi kabla ya kupokezwa mifugo hiyo baada ya wazee wa ukoo wa Aambua kusema wanashughulikia kesi nne zilizowasilishwa kabla ya kesi yao.

“Wakati wa mkutano Jumamosi, wazee hao walituambia tusubiri hadi mwaka wa 2023 ili kesi yetu itatuliwe kwa sababu wana kesi nne za kutatua,” akasema babake marehemu, Silu Mutua wakati wa mahojiano katika kijiji cha Mulili Jumapili iliyopita.

Wakati wa mahojiano hayo Mzee huyo mwenye umri wa miaka 94 alikuwa amezama katika lindi la mawazo kuhusu maisha ya marehemu mwanawe akiwa vile vile anaelekea kuwa kipofu kutokana na umri wake mkubwa.

Bw Sila alifariki baada ya makabiliano na Musyoka Kituku aliyemlipa Sh50 ili amshone mkoba lakini akafeli kuwajibika kwa muda walioagana.

Alifariki muda mfupi baada ya mapigano hayo huku mshukiwa akitoroka mji wa makindu kutokana na hofu ya kukamatwa.

Lakini siku chache baadaye, Bw Kituku alijiwasilisha katika kituo cha polisi cha makindu alikozuiliwa ingawa hakushtakiwa alipojitetea kwamba marehemu alianguka na kupata majeraha wala hakuchangia kifo chake.

Wakati mwili wa marehemu bado ukiwa katika mochari ya hospitali ya Makindu, Kituku Kitonde, babake mshukiwa aliwakusanya wazee wa ukoo wa Aambua, jamaa, marafiki na wanachama wa kundi la kibiashara la Makindu kisha akaanzisha mchakato wa siri wa kumwokoa mwanawe mikononi mwa polisi kwa kutumia tamaduni ya ‘Maambo’.

“Nilikubali kukumbatia maelewano nje ya mahakama kwasababu sikutaka kesi ambayo ingemhukumu mtoto wa rafiki yangu. Mimi ni mkiristo na dini pia hutoa nafasi ya msamaha,” akasema Mzee Mutua ambaye ni muumini wa dhati wa kanisa Katoliki.

Cha kushangaza ni kwamba siku mbili baada ya mazishi ya Bw Sila, mshukiwa aliwachiliwa huru kutokana na ukosefu wa ushahidi.

“Ingawa tumemwachilia, faili yake iko wazi na iwapo mashahidi watajitokeza basi tutaendelea na kesi,” akasema OCPD wa Makindu, Bw Peter Ochorokodi.

Hata hivyo ukoo wa Aambua haujatimiza ahadi ya kuwasilisha mifugo wote sita baada ya makataa ya mwezi Agosti kupita wakiwa wametoa ng’ombe moja tu.

You can share this post!

Wakazi wafurahia minofu ya bure lori kukanyaga kondoo 48

TAHARIRI: Mgomo utahujumu maandalizi shuleni

adminleo