• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
USHURU: Uhuru alivyotegwa

USHURU: Uhuru alivyotegwa

Na BENSON MATHEKA

IMEJITOKEZA kuwa wabunge walifanyia mabadiliko sheria ya fedha ili kumsukumia mzigo Rais Uhuru Kenyatta nao kujiondolea lawama kuhusu gharama ya maisha, wakiwa na ufahamu kwamba Kenya inashinikizwa kutoza kodi hiyo ya VAT ya mafuta ya asilimia 16.

Ni katika mazingira haya ya kusukumwa kwenye mwamba ambapo Rais Kenyatta amekuwa kimya tangu aliporejea nchini Jumapili kutoka ziara ugenini na amekuwa akishauriana na maafisa wake kutafuta suluhisho ambalo litawapa wananchi afueni, na wakati huo huo kudumisha urafiki na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Benki ya Dunia.

Mnamo Agosti 30, wabunge walifanyia mabadiliko Sheria ya Fedha ili kuahirisha ushuru uliopendekezwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich kwenye bajeti. Walifanya hivyo siku mbili tu kabla ya kuanza kwa utozaji wa VAT hiyo hapo Septemba 1.

Mara baada ya kupitisha mabadiliko ya kuahirisha utekelezaji wa ushuru huo hadi 2020, wabunge walienda mapumzikoni huku wakimtaka Rais Kenyatta, aliyekuwa China kwa ziara rasmi wakati huo, kuweka sahihi ili ushuru huo usitozwe hadi 2020.

Waziri Rotich aliposisitiza kuwa ni lazima ushuru huo utekelezwe kwa sababu mswada haukuwa umewekwa sahihi, wabunge walianza kulaumu Serikali wakisema inawanyanyasa raia wake na kumshinikiza Rais Kenyatta kupunguza mzigo wa gharama ya maisha kwa kuweka sahihi.

Wabunge walichukua fursa ya kila kikao na vyombo vya habari kutoa mwito kwa Rais “kuwaokoa Wakenya” na hivyo kutoa picha kwa Wakenya kuwa wao ndio watetezi wa wanyonge.

Wadadisi wa masuala ya uchumi wanahisi kwamba wabunge walipitisha mabadiliko yaliyowasilishwa na Kiranja wa Wachache Junet Mohamed ili waonekane kuwa wanatetea wananchi na kumuacha Rais kubeba mzigo wa lawama akikosa kutia sahihi mswada huo.

Kulingana na mtaalamu wa uchumi Kwame Owino, wabunge walipitisha mswada huo wakifahamu kuwa ushuru huo ulitokana na masharti ya Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF).

Unafiki wa wabunge pia unajitokeza kutokana na vile walivyosubiri hadi dakika ya mwisho kujadili suala hilo, ikizingatiwa kuwa Waziri Rotich alitangaza mipango ya kutoza ushuru huo Juni, lakini wabunge hawakulijadili. Iwapo wangepitisha awali wangempatia Rais muda wa kutafakari na kutafuta suluhisho.

Bw Mohammed, ambaye aliwasilisha mswada huo, alisema baada ya wabunge kuupitisha kwamba lilikuwa sasa ni jukumu la Rais kuwalinda raia kwa kutia sahihi sheria hiyo.

“Suala hili haliko katika mikono ya Bunge sasa. Wabunge walitoa msimamo wao kuhusu mswada huo katika chumba cha mjadala na kupitisha kwa pamoja kuahirisha utekelezaji wa ushuru huo,” alisema Bw Mohammed.

Hii haikuwa mara ya kwanza Bunge kukataa mapendekezo ya IMF jambo ambalo wadadisi wanasema linaweza kuathiri uchumi wa Kenya iwapo shirika hili litaichukua hatua.

Lucie Villa, mtaalamu wa uchumi wa shirika la Moody, ambalo mapema mwaka huu lilionya Kenya dhidi ya kujilimbikizia madeni mengi, alisema hatua ya wabunge inaweza kutumbukiza nchi katika msukosuko wa kifedha kwa sababu ya madeni.

Kulingana na shirika hilo, hatua ya Bunge ni hatari kwa sababu Kenya ilikuwa tayari imeahidi IMF kwamba ingeanza kutekeleza VAT hiyo kuanzia Septemba 1.

Hii ilijiri baada ya wabunge kukataa sharti lingine la IMF kwa serikali ya Kenya la kuondoa viwango vya riba.

Wabunge hao wamesukuma serikali kwa kona ikizingatiwa kuwa imani ya mashirika ya fedha ulimwenguni kwa Kenya inaweza kupungua na yaliyoikopesha kudai madeni yote na riba juu yake na kufanya nchi kukwama kiuchumi.

Madeni ya Kenya kutoka mataifa ya kigeni yamegonga Sh5 trilioni na wadadisi wanasema yanatokana na ushauri mbaya kuhusu masuala ya kiuchumi. Wadadisi huru wanalaumu Wizara ya Fedha kwa kutomshauri Rais ipasavyo kuhusu hatari ya nchi kuwa na madeni mengi.

Waziri Rotich amenukuliwa mara kwa mara akisema Kenya ina uwezo wa kulipa madeni yake yote akisisitiza inakopa kufadhili miradi yenye manufaa.

“Tunaweza kulipa madeni yetu bila tatizo la hofu ya kufilisika,” Bw Rotich alisema mapema mwaka huu.

Hata hivyo, presha imeongezeka kufuatia ushuru mpya wa mafuta ambao wabunge wanataka Rais kukubali kuahirisha wakisema utasababisha mfumko wa gharama ya maisha.

Jana, Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli alisisitiza kuwa kuna haja ya ushuru huo kuondolewa ili kuokoa Wakenya.

Mnamo Februari mwaka huu, Moody ilishusha Kenya kutokana na mzigo wa madeni.

You can share this post!

Harakisheni kuchunguza mauaji ya Sharon – Gavana Obado

Mtoto wa marehemu Sharon kuzikwa Alhamisi

adminleo