• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
BELACHEW GIRMA: Mwanamume anayeweza kucheka kwa saa tatu mfululizo

BELACHEW GIRMA: Mwanamume anayeweza kucheka kwa saa tatu mfululizo

MASHIRIKA  NA GEOFFREY ANENE

KICHEKO chako kinaweza kudumu saa ngapi? Pengine unadhani swali hili ni la kipuzi, lakini kutana naye Belachew Girma, mshikilizi wa rekodi ya kicheko kirefu duniani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la SABC, Muethiopia huyu anaweza kucheka saa tatu na dakika sita.

Shirika hilo linasema Belachew hata ameanzisha shule ya kufunza Waethiopia kufukuza huzuni zao kupitia kicheko inayofahamika kama Laughter for All Association Ethiopia (LFAE). “Belachew Girma ni gwiji wa kucheka duniani. Alipata taji hili baada ya kucheka saa tatu na dakika sita na kuweka rekodi hiyo.

“Anaendesha shule ya kucheka kwa wale wangependa kucheka kwa mioyo yao anavyofanya.

“Zaidi ya miaka 20 iliyopita, hata hivyo, yeye mwenyewe hakuwa na sababu ya kucheka. Baada ya kupoteza mke wake kutokana na ugonjwa wa ukimwi, aliingilia ulevi na utafunaji wa miraa. Maisha yake yalikuwa bila matumaini na ya upweke.

“Anasema mambo yalibadilika kabisa pale aliposoma kitabu kuhusu uchekaji na kujifunza jinsi ya kucheka bila sababu yoyote,” shirika hilo lilieleza. Girma, SABC inasema, anaamini kicheko ni kichocheo cha watu kufanya kazi.

“Ameanzisha shule ya kwanza kabisa barani Afrika ya kucheka ili kufundisha watu kucheka bila ya kujali shida wanazopitia. Kila Jumamosi, Girma na wanafunzi wake hupanda juu ya paa ya orofa nne jijini Addis Ababa kufanya mazoezi ya kucheka,” shirika hilo lilisema.

You can share this post!

Ingwe kujaribu kukata kiu ya ushindi ikikutana na Rangers

KRA yafunga akaunti za benki za FKF kwa kulemewa kulipa...

adminleo