• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
KURUNZI YA PWANI: Kizazi cha watumwa kijijini Freretown chadai haki yao

KURUNZI YA PWANI: Kizazi cha watumwa kijijini Freretown chadai haki yao

KAZUNGU SAMUEL na PHILIP MUYANGA

KIJIJI cha Freretown kilicho katika barabara kuu inayotoka Mombasa kwenda Malindi kina historia kuhusiana na biashara ya watumwa.

Almaarufu kama Frere, kijiji hicho kina historia ya kusitiri baadhi ya watumwa ambao walikuwa wamenaswa wakati wa kilele cha biashara hiyo katika karne ya 18.

Mzee Fredrick Uledi, 86 anayeishi katika kituo cha magari cha Kisimani anafahamu vyema historia ya eneo hilo la Freretown.

Hata hivyo kutokana na tatizo la kutosikia vyema, aliamua kutuunganisha na mjombake, Bw Price Uledi ili atupashe tulichotaka kujua.

Bw Uledi ambaye ni mwenyekiti wa muungano wa jamii ya Wafrere aliwasili akiwa ameandamana na katibu, Bw Jimmy Kitao.

Mzee Uledi ni miongoni mwa vizazi vya watumwa ambao waliachwa katika kijiji hicho wakati wa biashara ya utumwa.

“Sisi tunatoka katika jamii ndogo na tunabaguliwa sana. Kila mahali tunapoenda kutafuta huduma, utasikia watu wakisema kuwa sisi ni Wafrere na sio Wakenya kamili,” akasema Bw Uledi.

Aidha, alisema kuwa kijiji hicho kilianzishwa mwaka wa 1928 na utawala wa Uingereza kama kituo cha kuwahifadhi watumwa ambao hawakupata nafasi ya kupelekwa India na mataifa mengine.

“Wengi wa watumwa walikuwa wakitoka katika maeneo ya Kusini mwa nchi ya Tanzania, nchi ya Rhodesia (sasa Zimbabwe) na Malawi. Waarabu waliokuwa wakifanya biashara hiyo ya watumwa walikuwa wakiingia vijijini na kuwakamata watumwa. Baadaye waliwauza katika soko kuu la biashara hiyo katika eneo la Zanzibar,” akasema Bw Uledi.

Aliongeza kwamba wakati biashara ya utumwa ikimalizika, utawala wa Waingereza uliamua kuwachukua baadhi ya watumwa na kuwaweka katika kijiji cha Freretown kilichokuwa chini ya himaya ya Waingereza.

“Kabla ya eneo hili kununuliwa na Waingereza ili kuwahifadhi, watumwa waliokuwa wakipelekwa katika mataifa mbalimbali ikiwemo India.

“Hata hivyo baada ya biashara hiyo ya utumwa kupigwa marufuku, ndipo kukawa na makubaliano kati ya utawala wa Uingereza na Sultani wa Zanzibar kununua ekari 663 za ardhi kuwahifadhi watumwa waliokuwa wamekwama Mombasa,” akasema Bw Uledi.

Hata hivyo kulingana naye, jamii hiyo imekosa haki kwa zaidi ya karne moja sasa, na kwamba wamepokonywa baadhi ya ardhi ambayo walikuwa wakisimamia.

“Sisi wakazi wa Freretown tunasahauliwa. Kuna dhuluma nyingi ambazo bado tunapitia. Baadhi ya jamii zilizoko jirani zinaamini kwamba sisi tulipendelewa na utawala wa wazungu hivyo bado wanatutenga,” akasema.

Kwa sasa, yeye anatayarisha historia ya eneo hilo pamoja na biashara hiyo ya utumwa ili kuelimisha kizazi cha sasa.

Alisema kuwa hatima ya baadaye ya kijiji cha Freretown pia haijulikani baada ya nyumba za kisasa kujitokeza na kuzima muundo wa nyumba za kizamani ambazo walikuwa wakijenga.

“Nyumba ambazo tulikuwa tukijenga zilikuwa za vyumba viwili na sebule moja pekee. Lakini sasa nyumba kubwa zinaendelea kujengwa na kuharibu mpangilio wa eneo letu,” akasema.

Naye Bw Kitao alisema kuwa kama jamii, walikuwa wakisimamia taasisi kadhaa kama vile kanisa, shule na maeneo mengine ya burudani lakini sasa yote yamechukuliwa na serikali.

Na sasa vizazi hivyo vinataka vitambuliwe kama jamii zingine kama Wamakonde katika kaunti ya Kwale na Wanubi katika eneo la Kibra, Nairobi.

“Tunahisi kwamba tunatengwa lakini naamini kwamba kila kitu kitabadilika na serikali itasikia kilio chetu,” akasema Bw Uledi.

Wakili Gunga Mwinga, jamii hiyo kwanza inafaa kujikubali kama jamii ndogo kisha baadaye iandikie bunge ikitaka kutambuliwa.

“Mbali na hilo, jamii hiyo vile vile inaweza kumuandikia Rais Uhuru Kenyatta moja kwa moja ikitaka kutambuliwa kama jamii,” akasema Bw Mwinga.

You can share this post!

KURUNZI YA PWANI: Wanawake wajipa ujasiri kupinga ukeketaji

TAHARIRI: Madiwani wakome kutatiza maafisa

adminleo