• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Wabunge waapa kuangusha pendekezo la ushuru wa mafuta

Wabunge waapa kuangusha pendekezo la ushuru wa mafuta

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Jumanne waliendelea kupinga pendekezo la Rais Uhuru Kenyatta la kutaka mafuta yatozwe ushuru wa ziada ya thamani (VAT) ya kima cha asilimia 8, wakisema ushuru huo utawaumiza zaidi Wakenya wanaozongwa na mzigo mzito wa gharama ya maisha.

Wabunge hao kutoka mirengo ya Jubilee na NASA walisusia mikutano iliyoitwa na viongozi wao ili kuwashawishi kuunga mkono suala hilo pamoja na kupunguzwa kwa bajeti za bunge na hazina ya maendeleo katika maeneo bunge (CDF).

Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Bw Simba Arati alisema anamuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na ajenda zingine muhimu kama vita dhidi ya ufisadi anapinga vikali ushuru wa VAT kwa bidhaa za mafuta.

Mbunge wa Borabu Innocent Obiri Momanyi alipohojiwa na wanahabari Septemba 18, 2018 nje ya majengo ya Bunge, Nairobi. Picha/ Charles Wasonga

“Ushuru kama huu utawaumiza Wakenya ambao tayari wanazongwa na kupanda kwa gharama ya maisha. Hii ndio maana tunaipinga vikali kwani sasa ni wawakilishi wa wananchi hao,” akasema.

Bw Arati aliitaka serikali kubuni njia zingine za kusaka pesa za kufadhili miradi ya maendeleo pamoja ikiwa ni pamoja na kuimarisha vita dhidi ya ufisadi.

“Kwa rais anafa kuziba mianya ya wizi wa fedha za umma iliyoko katika afisi yake na bila shaka atapata pesa za maendeleo badala ya kuendelea kuanzisha ushuru mwingine kwa Wakenya,” akasema Bw Arati ambaye ni Mbunge wa ODM.

Na Mbunge Maalum Bw Godffrey Osotsi alisema atapinga VAT kwa mafuta kwa sababu hatua hiyo itaathiri ukuaji wa uchumi wa nchini.

“Badala ya Serikali kutoza Wakenya ushuru wa VAT kwa mafuta,, serikali inafaa kupunguza bajeti za mipango isiyo muhimu kama ule ya kuwanunulia wanafunzi wa shule za msingi vipakatalishi. Mpango huu umekuwa ukitengewa mabilioni ya fedha kila mwaka lakini kufikia sasa watoto wetu hawatumii vifaa hivyo,” akasema Bw Osotsi ambaye ni Mbunge wa chama cha ANC.

Alisema Sh52 bilioni ambazo serikali inalenga kukusanya kupitia VAT kwa mafuta ni pesa kidogo ambayo serikali inaweza kupata ikiwa itapunguza bajeti ya mipango isiyo ya maana na dharura.

Mbunge Maalum wa chama cha ANC Godfrey Osotsi alipohojiwa na wanahabari Septemba 18, 2018 nje ya majengo ya Bunge, Nairobi. Picha/ Charles Wasonga

Bw Ososti alisema shida kubwa katika serikali hii ya Jubilee ni wizi wa pesa za umma na hamu ya kukopa pesa za maendeleo kutoka mataifa ya nchini.

“Serikali hii inafaa kuiga mfano wa Rais mstaafu Mwai Kibaki ambaye aliweza kuendesha uchumi bila kukopa pesa nyingi kutoka mataifa ya nje,” akasema.

Mbunge wa Bobasi Bw Innocent Obiri Momanyi (PDP) alisema serikali inafaa kukumbatia mtindo ya matumizi mazuri ya rasilimali ili kuzuia wizi na ubadhirifu.

Vincent Mogaka, mbunge wa Mugirango Magharibi alipohojiwa na wanahabari Septemba 18, 2018 nje ya majengo ya Bunge, Nairobi. Picha/ Charles Wasonga

“Usimamizi mbaya wa rasilimali za umma, unaotoa mwanya wa wizi, ndio tatizo kuu linaloizonga taifa hili. Hii ndio maana sasa serikali inageukia mwananchi wa kawaida kwa kumtoza ushuru wa juu. Tunapinga hatua kwa sababu tulichaguliwa kulinda masilahi ya wananchini,” akasema Bw Obiri.

Naye Mbunge wa Mugirango Magharibi Vincent Mogaka alimkosoa Rais Kenyatta kwa kutoa mapendekezo kuhusu ushuru wa VAT kwa mafuta bila kushauriana na wabunge.

“Sisi ndio wawakilishi wa wananchi na ilifaa Rais atushauri kwanza kabla ya kuleta mapendekezo yake bungeni. Tutapinga mapendekezo ya rais kwa misingi hii,” akasema Mbunge huyo wa chama cha Ford Kenya.

Godfrey Osotsi aliposema Sh600 bilioni hupotea kwa ufisadi kila mwaka. Picha/ Charles Wasonga

Mwenzake wa Bomachoge Chache Alfa Miruka Ondieki alisema ni makosa kwa serikali kupunguza mgao wa fedha za CDF kwa kima cha Sh6 bilioni akisema hatua hiyo itanyima maeneo bunge pesa za maendeleo.

“Hatua ya kupunguzwa kwa fedha za CDF inaonyesha kuwa serikali hii haijali masilahi ya Wakenya ambao wamekuwa wakifaidi kutokana na miradi ya maendeleo kupitia hazina hiyo,” akasema.

Kauli yake iliungwa mkono na Mbunge wa Matungulu Stephen Mule ambaye alialalamika kuwa tayari wao kama wabunge walikuwa wamepangia pesa za hazina hiyo katika mwaka huu wa kifedha wa 2018/2019.

Innocent Obiri anapendekeza matajiri watozwe ushuru wa juu kuliko wananchi wa kawaida. Picha/ Charles Wasonga

“Swali langu ni je, kwa kupunguza Sh6 bilioni kutoka kwa CDF, serikali inataka tupate pesa wapi za kutekeleza maendelea ambayo tayari wananchi walikuwa wameahidiwa?” akauliza Bw Mule ambaye ni Mbunge wa Chama cha Wiper.

Mbunge wa Baringo ya Kati Bw Joshua Kandie alisema alikataa kuhudhurua mkutano wa kundi la wabunge wa Jubilee uliotishwa na Rais Kenyatta kwa sababu ushuru VAT utawaumiza wananchi hao.

“Watu wangu wa Baringo ya Kati walinutuma bungeni niwatetee wanapoumia. Na ni wazi kuwa wengi wao wamekuwa wakiumia tangu serikali ilipoanza kutekeleza utozaji wa ushuru huo wa mafuta. Hii ndio maana sikuhudhuria mkutano huo ambao ulilenga kuwaumiza hata zaidi,” akasema Bw Kandie ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Chap Chap.

Joshua Kandie, mbunge wa Baringo ya Kati alipohojiwa na wanahabari Septemba 18, 2018 nje ya majengo ya Bunge, Nairobi. Picha/ Charles Wasonga

Naye Mbunge wa Sigowet/Soin Kipsengeret Koros alisema anapinga VAT kwa mafuta kwa sababu ya kujitolea kwake kusimama na Wakenya.

“Hili suala halihusu chama changu cha Jubilee bali linawahusu Wakenya. Hii ndio maana leo (Jumanne) nilikataa kuhudhuria mkutano uliotishwa na kiongozi wa chama changu Rais Kenyatta katika Ikulu ya Rais,” akasema Mbunge huyo anayehudumu kipindi cha kwanza.

Bw Koros pia alipinga hatua ya serikali kuanzisha ushuru wa kuchangia hazina ya kufadhili ujenzi wa nyumba za gharama za chini ili kuafikia lengo la mojawapo ya nguzo nne kuu za serikali.

Bw Kandie na mbunge wa Matungulu Stephen Mulee (kati) walipohojiwa na wanahabari Septemba 18, 2018 nje ya majengo ya Bunge, Nairobi. Picha/ Charles Wasonga

Akasema: “Suala la nyumba sio la dharura sasa. Ushuru huu unaweza kutozwa wakati mwingine. Kile Wakenya wanahitaji wakati huu ni njia za kupunguza gharama ya juu ya mahitaji yao ya kimsingi.”

Wabunge tuliozungumza nao na kupinga mapendekezo ya serikali walielezea matumaini yao kuwa ikifikapo Ijumaa watakuwa wamepata idadi ya wabunge 233 ili kuweza kuangusha memoranda ya Rais Kenyatta.

Kufikia sasa wabunge ambao wapinga ushuru huu dhalimu ni 260. Naamini kuwa ifikapo Alhamisi idadi hii itafika wabunge 300,” akasema Bw Arati.

  • Tags

You can share this post!

Shirika lataja Reggea kama kikwazo kwa elimu ya watoto

Historia yajirudia Raila Odinga Junior akimpinga...

adminleo