• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
Historia yajirudia Raila Odinga Junior akimpinga ‘Baba’

Historia yajirudia Raila Odinga Junior akimpinga ‘Baba’

Na PETER MBURU

MWANAWE kiongozi wa upinzani Raila Odinga amejitokeza mbele ya umma kumpinga babake pamoja na upinzani kwa kuunga mkono kutekelezwa kwa sheria ya ushuru wa mafuta, akisema hata matakwa yaliyowekwa na muungano wa Nasa hayawezi kutimizika.

Raila Odinga Junior, alianza kuponda upande wa upinzani punde walipotoa habari kwa umma kuwa wameamua kuunga mkono sheria hiyo, licha ya wabunge wa muungano huo mbeleni kusema hawataiunga mkono.

“Kwa bahati mbaya kama raia wa Kenya sijaridhishwa na ujumbe wa Nasa kuhusu suala la ushuru wa VAT kwa mafuta, kati ya matakwa waliyoweka hakuna linaloweza kupimika na hata kama yangepimika hayawezi kusaidia kuokoa mzigo wa deni. Naomba mbunge wangu @okothkenneth kupinga,” Raila junior akasema kupitia akaunti yake wa Twitter Jumanne.

Maneno yake yalifuatwa na hisia tofauti kutoka kwa Wakenya, wengi wakitabiri kuwa ameanza kumkaidi babake, ambaye aliongoza kikao cha wabunge wa Nasa waliofikia uamuzi huo, na kujaribu kuvuta kumbukumbu za wakati Raila Odinga alimpinga babake Oginga Odinga miaka ya zamani.

Brigadier General @BrigadierBrigad alisema “Historia inajirudia, Raila alimpinga babake Jaramogi na sasa Raila Jr anakinzana na Raila Sinia wazi kuhusu hatua ya ushuru wa VAT. Mbaya sana.”

Musamali  @austinmusamali naye alimkosoa Raila Jr akisema “Lakini mkutano huo uliongozwa na babako, ulimwomba yeye kupinga kabla hajatoka nyumbani?”

“Lakini babako aliwalazimisha wabunge hao kuunga mkono mapendekezo, kile tu ulihitaji kufanya ni kuzungumza na babako,” Douglas Buluma @OkukuDouglas akamjibu Raila Jr.

Na japo Wakenya wengine kama Philosopher @Philosopher254 walikuwa na maoni kuwa Raila Jr anamtega mbunge wake Kenneth Okoth ili akimpinga babake atemwe katika uchaguzi ifikapo 2022 naye Raila Jr aingizwe hapo, wengi wa Wakenya ni wale walioshangaa namna kijana huyo ameamua kwenda kinyume na babake.

Jumatano alfajiri, Raila Jr alidamka na ujumbe huohuo, akiwataka Wakenya kutumia mitandao ya kijamii kuzungumza na wabunge wao kuwarai wasiunge mkono sheria ya ushuru wa VAT.

“Jana niliandikia mbunge wangu nikimtaka kupinga mapendekezo kwenye sheria ya ushuru wa VAT, watu wengi walijibu. Ikiwa unataka kutumia mitandao ya kijamii kupaza sauti vyema, zungumza moja kwa moja na mbunge wako kama nilivyofanya. #Kenyansfirst,” akachapisha.

You can share this post!

Wabunge waapa kuangusha pendekezo la ushuru wa mafuta

Waliokwepa kulipa ushuru wa Sh50 milioni waitwa kortini

adminleo