• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Uhuru akwepa ghadhabu za Wakenya walio Amerika

Uhuru akwepa ghadhabu za Wakenya walio Amerika

NA CHRIS WAMALWA

RAIS Uhuru Kenyatta hana mpango wa kukutana na Wakenya wanaoishi Amerika akiwa nchini humo kuhudhuria Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) litakalofanyika Jumanne. 

Baadhi ya Wakenya wanaoishi Amerika walitarajia kumwuliza maswali Rais Kenyatta kuhusu matukio mbalimbali ya kitaifa ikiwemo ongezeko la ushuru kwa bidhaa muhimu.

Kulingana na Balozi wa Kenya nchini Amerika, Bw Robinson Githae, ubalozi huo na Wizara ya Mashauri ya Kigeni hazijapanga mkutano wowote kati ya Rais na Wakenya walio Amerika.

“Ninavyojua, hakuna mipango yoyote kama hiyo kwani rais atakuwa anahudhuria mikutano mingi mno na viongozi wa mataifa mengine pamoja na washirika wa maendeleo akiwa New York,” akasema Bw Githae.

Wakenya wengi wanaoishi Amerika wamekuwa wakiuliza Rais atakutana nao lini na wapi, kwani ilikuwa desturi miaka iliyopita kwa rais kukutana nao akiwa nchini humo.

Endapo Rais Kenyatta hatabadilisha mipango yake na atenge muda kukutana na Wakenya hao, hii itakuwa mara yake ya pili kutokutana nao anapozuru Amerika kwa chini ya mwezi mmoja.

Mwezi uliopita, Rais alikuwa Washington kwa ziara ya siku mbili ambapo alikutana na Rais Donald Trump katika Ikulu ya White House.

Wachanganuzi walisema huenda Rais anaepuka maswali mengi kutoka kwa Wakenya walio nchini humo, hasa wakati huu kufuatia mswada wa fedha uliopelekea ongezeko wa ushuru kwa bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta.

“Rais alikuwa hatarini kukabiliwa na maswali chungu nzima kama si kuzomwa na Wakenya walio ughaibuni ambao huwa hawatishwi na mamlaka ya Rais jinsi ilivyo nyumbani. Wengi walikuwa wamepanga kumuuliza maswali mazito mno,” akasema Dkt Duncan Obare, kutoka Manchester, New Hampshire.

Naye Bw Said Ali Badawy kutoka Maryland, alisema ushuru uliopitishwa utaathiri pia Wakenya wanaoishi ng’ambo kwani wana jamaa zao ambao huwategemea humu nchini.

“Inamaanisha Wakenya walio ughaibuni watalazimika kutuma hela zaidi kusaidia jamaa zao nyumbani. Mswada huu uliopitishwa kwa njia za kilaghai unaathiri pia Wakenya wanaoishi ng’ambo,” akasema, kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Kongamano kuu la 73 la UN lilifunguliwa mnamo Septemba 18, lakini mkutano wa kwanza wa viongozi wa mataifa utaanza kesho. Kongamano linatarajiwa kufanyika kwa siku tisa.

Bw Githae alisema Rais Kenyatta amepangiwa kugusia masuala ya ushirikiano wa kimataifa, usalama na amani, kutetea uongozi wa vijana na ujasiriamali, kutangaza nafasi za uwekezaji Kenya na uzinduzi wa safari za moja kwa moja za shirika la ndege la Kenya Airways kutoka Nairobi hadi new York.

You can share this post!

Wafuasi wa Obado sasa waandamana wakitaka aachiliwe huru

Juhudi za kumng’oa Spika Muturi, Duale na Mbadi zaanza

adminleo