• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Uweza Queens inavyowapa vipusa fursa ya kunoa makali yao

Uweza Queens inavyowapa vipusa fursa ya kunoa makali yao

Na PATRICK KILAVUKA

UWEZA Queens, timu ya soka ya wanadada inayotesa mtaani Kibra, Nairobi ilistawishwa mwaka 2017.

Ina kikosi cha wachezaji kumi na tisa ambao wananolewa katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Toi na kupigia michuano ya ligi ya FKF, kinadada ya Kanda ya Nairobi (NWL) uwanja wa Woodley.

Kikosi cha Uweza Queens Kibra kikiingia uwanjani kucheza dhidi ya Archivers Ladies uwanjani Kihumbuini. Picha/ Patrick Kilavuka

Iliazimia kuwapa vipusa fursa ya kusakata kabumbu katika mazingira yafaao na kubadilisha maisha yao kupitia kutumia vipaji vya masomo na talanta.

Malengo ya timu hii yanaonekana kutimia kwa sababu wasichana ambao wamebahati mithili ya mtende, hupata elimu ya shule ya msingi na ya upili kupitia mpango maalum wa ufadhili kupitia Uweza. Hata wengine hupata fursa ya kucheza soka ughaibuni.

Kikosi cha Uweza Queens Kibra kikisalimiana na wapinzani Archivers Ladies kabla mchuano kuanza uwanjani Kihumbuini. Picha/ Patrick Kilavuka

Miongoni mwa wale ambao wameonja tayari matunda hayo ya kukuza talanta ni Matilda Muhonja ambaye amewahi kutalii Uholanzi baada ya kupata ufadhili akiwa kidato cha pili Shule ya Upili ya Kibuon, Kaunti ya Migori.

Wengine ambao wanafadhiliwa na Uweza baada ya huduma zao za kandanda kunaswa na kupigia chapuo taaluma yao ya soka ni Medina Abubakhari (miaka 12), Siama Mohammed, Joyce Wanuna (Shule ya upili ya Kibuon) miongoni mwa wengine.

Kikosi cha Uweza Queens Kibra kikicheza dhidi ya Archivers Ladies uwanjani Kihumbuini.Picha/Patrick Kilavuka

Wanaisifia kuwa mkombozi wa maisha yao kwa kuwalipia karo. Fauka ya hayo, imewawezesha kujiepusha na marafiki wabaya, madawa na hata kuwa zizi mbadala la kuleta matumaini katika maisha yao.

Uweza inalenga wasichana wapevu masomoni kuendeleza ndoto ya kupata elimu wakikuza vipawa vyao vya kabumbu. Japo kwa kuthamani pia vipaji adimu, wale ambao wameruzukiwa hawajasazwi wanaporidhisha Uweza kwamba, vipawa vyao vya soka vina makali lakini wanakosa kupata fursa kuvichochea au kuviangazia.

Mchezaji Medina Abubakhari( mwenye kofia) akipambana kuwahi boli.Picha/Patrick Kilavuka

Malengo mingine ambayo yanakumbatiwa ni kuwanidhamisha, kuwakuza kimaadili, kuwatahadharisha na mimba za mapema na kadhalika.

Chini ya benchi ya kocha Dennis Odhiambo (mchezaji wa zamani wa timu ya madume ya Uweza) na timu meneja Charles Khaindi imepimwa uwezo wake kupitia kusajiliwa katika ligi iliyotajwa awali.

Kikosi cha Uweza Queens, Kibra kikisherekea baada ya kufunga bao dhidi ya Archivers Ladies uwanjani Kihumbuini. Picha/ Patrick Kilavuka

Kufika kuandika kwa makala, ilikuwa imejitosa ugani mara tano. Iliichabanga Kibagare Girls 2-1 kabla kuilipua Archivers Ladies 2-1 uwanjani Kihumbuini.

Hata hivyo, ilipigwa katika mechi yake dhidi ya Kangemi Ladies 1-0, kukomolewa na Beijing Raiders 2-0 ugani Mathare Depot kisha kusazwa na Amani Queens 2-0 katika mechi ambayo ilipepetewa uwanja wa Nakeel.

Mchezaji Matilda Muhonja(5) akionyesha miondoko yake ya kupiga chenga. Picha/Patrick Kilavuka

Wachezaji ambao walisajiliwa kupiga jeki kikosi in kipa Joy Adhiambo, madifenda Warda Mayungi na Anne Aanyango na mastraika Cindy Aluoch na Susan Kwamboka

Mipango ya timu sasa ni kujiimarisha zaidi kupanda ngazi ya ligi ya daraja ya juu na kuendelea kulea talanta za wanasoka hawa ambao wamechongwa tangu wengine wakiwa na miaka ya chini ya miaka kumi na miwili.

Mashauriano baada ya mechi. Picha/ Patrick Kilavuka

You can share this post!

Mkenya aweka rekodi mpya Amerika Kusini mbio za kilomita 42

PATRICK OTIENDE: Straika wa Kangemi anayepania kufikia...

adminleo