• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Nyota wa Cameroon astaafu baada ya kocha kusema ligi ya Uchina ni ya kipuuzi

Nyota wa Cameroon astaafu baada ya kocha kusema ligi ya Uchina ni ya kipuuzi

Na GEOFFREY ANENE

Nahodha wa Cameroon, Benjamin Moukandjo ametangaza kustaafu kuchezea nchi hiyo baada ya kocha mpya Clarence Seedorf kusema wachezaji wanaosakata soka Uchina ama Bara Asia “hawatoshi mboga” kujumuishwa kikosini.

Moukandjo, ambaye alisaidia Indomitable Lions kutwaa taji la Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2017, anasakata katika klabu ya Beijing Renhe nchini Uchina, ambayo Mkenya Ayub Timbe pia anachezea.

Mholanzi Seedorf hakuita Moukandjo kwa mechi ya kufuzu kushiriki AFCON dhidi ya Visiwa vya Comoro, ambayo ilikamilika 1-1 Septemba 8, 2018.

“Wachezaji lazima waelewe kwamba iwapo watakimbilia donge nono, basi watapoteza nafasi zao za kuwakilisha taifa. Wachezaji wazuri vijana hawachezi nchini Uchina ama Bara Asia,” Seedorf alieleza mwezi Agosti 2018. “Hata hivyo, hatufungii mlango yeyote, tunataka wachezaji walio na nidhamu na bidii na kama kuna mmoja anayesakata soka yake Mashariki ya Kati na anaweza kudhihirisha uwezo wake uwanjani, tutamjumuisha kikosini.”

Baada ya matamshi ya Seedorf, Moukandjo, ambaye alitua nchini Uchina siku chache baada ya kuongoza Cameroon kushinda AFCON akitokea klabu ya FC Lorient nchini Ufaransa, alitoa taarifa akieleza sababu zake za kustaafu Septemba 23, 2018.

“Matamshi ya Bwana Clarence Seedorf yalifanywa kwa haraka na si ya haki. Si ya haki kwa sababu licha ya mimi kuwa nahodha, sikuwahi kupigiwa simu kujulishwa uamuzi wake…Uwezo wa mchezaji hutathiminiwa uwanjani kabla ya kocha kuamua kupuuza mchezaji yeyote… Nashukuru wote walionisaidia kufika hapa na ninaitakia Cameroon kila la kheri katika AFCON na ninatumai itaweza kuhifadhi taji,” mshambuliaji huyu alisema.

You can share this post!

Kaunti ya Nandi yamtuza Kipchoge ng’ombe, uwanja mpya...

GHARAMA YA MAISHA: Kejeli na matusi kwenye akaunti za Rais...

adminleo