• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Gavana Mutua apondwa kujifanya anahisi uchungu wa ‘Wanjiku’

Gavana Mutua apondwa kujifanya anahisi uchungu wa ‘Wanjiku’

Na PETER MBURU

GAVANA wa Machakos Alfred Mutua amekumbana na ghadhabu za Wakenya baada ya kujaribu kulalamika kuhusu kupandishwa kwa ushuru na matumizi mabaya ya serikali, walipomtaka kukoma kujifanya wakati hana tofauti na serikali.

Gavana Mutua alituma ujumbe kwenye akaunti yake ya Facebook Jumatatu akieleza namna serikali imekwenda mrama kwa kupandisha ushuru, lakini Wakenya wakamkemea kuwa anajifanya anahisi uchungu wa ‘Wanjiku’.

“Kupandisha ushuru wakati bado tunavuja upande mwingine, kupitia ufisadi na matumizi mabaya yay a pesa ni kuturudisha katika shida ya deni. Ni wazi kuwa nchi yetu inaishi zaidi ya uwezo wake haswa katika ujenzi wa nyumba na barabara.

Inashangaza kuwa tunajenga kilomita moja ya barabara kwa Sh1bilioni wakati karibu Sh600 milioni zinaharibiwa na kuibiwa. Teknolojia mpya zinaweza kutusaidia kupunguza matumizi haya kwa kiwango hadi cha asilimia 60,” Gavana Mutua akachapisha.

“Ninamrai Rais Uhuru Kenyatta kuunda jopokazi ya kukagua miradi hii ya pesa nyingiambayo hatuwezi kuigharamia, ilinganishe na miradi sawia katika mataifa mengine ya Afruka na Uropa na itoe suluhu ya hakika kwa tatizo hili kwani limemwadhiri mwananchi wa kawaida ambaye ana mzigo mkubwa kipesa. Lazima tuokoe nchi yetu na sote sharti tuwe sehemu yake,” akamaliza.

Lakini watumizi wa Facebook hawakupokea ujumbe wa gavana huyo kwa njia nzuri, wengi wakidai alikuwa akijifanya kuwa pamoja na Wakenya, ilhali anajifanya.

“Pia tunahitaji kaunti na maeneobunge kuunganishwa ili kupunguza mzigo wa mishahara. Kwa mfano tuunganishe Machakos na Makueni ndiposa Gavana Kivutha Kibwana awe gavana nawe usimamie idara yake ya mawasiliano kwa kuwa unapenda vichekesho na kujionyesha (PR),” AKASEMA Dalmas Mumo.

Nicholas Mwangangi alisema “Wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, ulijitokeza wazi kumuunga mkono Uhuru Kenyatta kuwa Rais. Usitumie hila zako za PR kwa Wakenya hapa. Tafuta muda uzungumze na Bw President moja kwa moja.”

Wengine walikosoa wazo la kutaka kuundwe jopokazi, wakisema historia iliyojiweka ni kuwa ripoti za mbeleni hazijawahi kutekelezwa.

 Lakini hata hivyo, kunao wachache ambao waliunga mkono wazo la gavana huyo, wakisema serikali imekuwa ikitumia kupita kiasi, wakati wananchi wanaishi maisha ya umaskini mkubwa.

You can share this post!

Wavumbuzi wa Instagram wajiuzulu ili wapumzike

Mezeni wembe, De Gea awafokea wakosoaji

adminleo