• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Taharuki Raila akipiga kambi mjini Migori

Taharuki Raila akipiga kambi mjini Migori

Na ELISHA OTIENO

TAHARUKI imetanda katika Kaunti ya Migori huku kinara wa ODM Raila Odinga akipanga kuenda kukita kambi katika eneo hilo kumpigia debe mwaniaji wa chama chake Ochilo Ayacko.

Wawaniaji wa useneta katika uchaguzi mdogo wa useneta utakaofanyika Oktoba 8, tayari wameonywa dhidi ya kuzua fujo.

Afisa Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Migori Joseph Nthenge alisema kwamba maafisa wa usalama wameagizwa kufuatilia kwa karibu mikutano ya kisiasa katika maeneobunge yote manane ili kunasa wanasiasa wanaochochea wananchi.

Fujo zilishuhudiwa katika siku za hivi karibuni na kuwaacha watu kadhaa wakiuguza majeraha.

“Sitajali hadhi yako katika jamii. Utakamatwa na kushtakiwa kwa kuzua fujo,” akasema.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati alionya kuwa wawaniaji watakaojihusisha na vurugu watazuiliwa kuwania.

“Kaunti ya Migori ni moja ya maeneo yaliyo na visa vya vurugu japo hatujapokea ripoti zozote kuhusiana na fujo hadi kufikia sasa,” akasema Bw Chebukati.

Bw Nthenge na Bw Chebukati walizungumza huku kukiwa na taharuki kutokana na ziara ya Bw Raila atakayezuru eneo hilo wiki hii.

Mwaniaji wa chama cha Federal Party of Kenya Eddy Oketch alisema kuwa tume ya IEBC imemruhusu kuendesha kampeni katika eneobunge la Suna Mashariki Oktoba 5.

Hiyo ndiyo siku ambayo Bw Odinga anatarajiwa kuhutubia mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Migori katika eneobunge la Suna Mashariki.

Bw George Maando, mwendesha kampeni za Bw Oketch, aliitaka IEBC na polisi kulazimisha chama cha ODM kuhamisha mkutano wao hadi katika uwanja wa shule ya msingi ya Migori iliyoko umbali wa kilomita 2 ili kuzuia kuzuka kwa fujo.

“Tunafaa kuheshimu ratiba ya kampeni iliyotolewa na IEBC ili kuepuka ghasia,” akasema Bw Maando.

Lakini Katibu Mkuu wa ODM tawi la Migori Joseph Olala alisema kwamba Bw Odinga ni kiongozi wa kitaifa ambaye ataenda katika eneo hilo kukutana na watu wa Migori na kueneza ‘injili’ kuhusu umoja wa kitaifa kwa mujibu wa mwafaka baina yake na Rais Uhuru Kenyatta.

“Kiongozi wa chama chetu atakuja kusalimia watu wa Migori na wala si kuendesha kampeni na hakuna yeyote atamzuia kufanya hivyo,” akasema Bw Olala.

Bw Odinga ambaye ataandamana na magavana, maseneta na wabunge wa ODM anatarajiwa kupiga kambi katika Kaunti ya Migori kati ya Oktoba 4 na Oktoba 5 ili kumpigia debe Bw Ayacko.

Chama cha ODM tayari kimekodisha uwanja wa Migori na hata kulipia ada inayohitajika.

Wapigakura 380,000 watakuwa wanachagua seneta siku ambayo Gavana Okoth Obado atakuwa anarejea katika Mahakama ya Milimani ili kujua hatima yake ikiwa ataachiliwa huru kwa dhamana.

Gavana Obado amekuwa akizuiliwa katika gereza la Industrial Area, Nairobi tangu kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji ya mwanafunzi wa Rongo Sharon Otieno ambaye maiti yake ilipatikana msituni Sepetemba 4 katika Kaunti ya Homa Bay.

Gavana Obado alikuwa anaunga mkono Bw Oketch katika kinyang’anyiro cha useneta.Bw Obado alitangaza msimamo wake wa kuunga mkono Bw Oketch baada ya chama cha ODM kuteua moja kwa moja Bw Mr Ayacko ambaye ni hasimu wake mkuu wa kisiasa.

You can share this post!

Pendekezo la kubadilisha Katiba lagawanya Jubilee

Walimu walalamikia kukatwa mishahara bila taarifa

adminleo