21/04/2019

Pogba au Mourinho, nani aondoke?

NA JOB MOKAYA

WIKI iliyopita, ulimwengu wote wa soka ulishuhudia tukio la kushangaza sana. Mitandao ya kijamii ilisheheni kanda ya video uliokuwa unaonesha kiungo wa kati wa Manchester United Paul Pogba akijibizana na meneja wake Jose Mourinho.

Kwenye kanda hiyo, Pogba anaonekana mwenye tabasamu tele anapopiga kwata huku akiwasalimu makocha wengine wa Man-United. Pindi anapofika kwa kocha wake Mourinho, Pogba anampuuza na kutomsalimu.

Kitendo hicho kinamuudhi Mourinho anayeonekana kusema jambo fulani, jambo ambalo linaelekea kumkasirisha Pogba.

Kisha, Pogba anaanza kujishashashasha kana kwamba hakuna wa kumtisha yeye. Kisha, Pogba anaelekea kwenye maegesho na kutia gari lake moto kisha kuondoka kwenye uwanja wa mazoezi bila idhini ya mkubwa wake.

Tukio hili la kutisha linatanguliwa na kichekesho kingine ambapo timu ya Man-United ilibanduliwa na limbukeni Derby County kwenye Kombe la Carabao, zamani likiitwa Carling Cup.

Ajabu ni kwamba Derby inacheza soka ya Daraja ya Pili, na mtanange huu ulipigwa katika uga wa Old Trafford. Aibu iliyoje kwa Mashetani Wekundu! Aibu iliyoje kwa Mourinho!

Baada ya mechi hii iliyoisha kwa sare ya 2-2 katika muda wa kawaida na kisha Man-United kushindwa 7-8 kwa penalti, Pogba anaweka video kwenye mtandao wa Instagram akipasua kicheko kikuu.

Ingawa nia ya kicheko chake haikujulikana haraka, mashabiki wengi waliotoa maoni chini ya video hiyo walimkashifu sana Pogba na kudai kwamba huenda alifurahia Man-United kunyukwa na Derby County mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Matukio haya ya wiki jana ni kionjo tu cha vituko, vimbwanga na sarakasi kati ya Pogba na Mourinho. Sasa, Pogba anataka kuondoka Man-United mapema Januari huku Barcelona ikimezea mate huduma zake.

Swali muhimu ni je, kati ya Pogba na Jose Mourinho, ni nani anafaa kuondoka Old Trafford? Tumeyasema ya Pogba, ya Mourinho ni yapi?

Huu ni msimu wa tatu wa Mourinho kambini mwa Man-United. Mourinho hajawahi kukaa kwenye timu moja zaidi ya misimu mitatu. Kwenye klabu zote alizofanyia kazi kama vile Porto, Inter Milan, Real Madrid na Chelsea mara mbili, Mourinho huondoka kwenye msimu wa tatu.

Kwenye misimu hiyo yote mitatu ambayo Mourinho aliondoka kwenye timu hizo, tayari alikuwa ameshinda angalau Ligi Kuu au Klabu Bingwa Ulaya (UEFA Champions League). Hivyo, hakuondoka kwa fedheha.

Kumbe si kila siku ni Jumapili. Pana Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi, Ijumaa na hata Jumamosi. Kwa mara ya kwanza, Mourinho anajikuta katika msimu wa tatu bila lolote la muhimu la kuonesha watu.

Kwa nini Mourinho hampendi Pogba? Jibu ni kwamba, Mourinho pia hampendi Anthony Martial, na hata hawapendi madifenda wake. Mourinho hampendi Pogba kwa sababu Pogba ana domo kaya. Kidomodomo kila mara. Kidomodomo ambacho hata kinamkashifu Mourinho mwenyewe hadharani.

Mourinho si kocha wa kwanza kuwa na mzozo na wachezaji wake nyota. Hata Guardiola hampendi Sergio Aguero ambaye ni nyota wa Manchester City. Pia hakumpenda kabisa Yaya Toure kwa sababu ya rangi ya ngozi yake. Hata kocha wa zamani wa Man-United Sir Alex Ferguson hakuwapenda wachezaji David Beckham na Cristiano Ronaldo hadi akawauza.

Kuhusu Mourinho na Pogba, nani aondoke nani abaki? Mmoja wao au wote? Pogba huenda akaondoka Januari, Jose sijui kama ataiwahi Januari yenyewe. Langu ni jicho, jicho tu!