• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 7:55 AM
Mbinu za kuiba mitihani ya KCPE na KCSE zaanikwa na serikali

Mbinu za kuiba mitihani ya KCPE na KCSE zaanikwa na serikali

Na LEONARD ONYANGO

WIZARA ya Elimu imefichua mbinu ambazo baadhi ya watahiniwa wanapanga kutumia ili kupata mwanya wa kuiba mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE).

Baraza la Mtihani nchini (Knec) limesema kuwa jumla ya shule 30 zinachunguzwa kwa kupanga njama za udanganyifu.

Katibu wa wizara ya Elimu Belio Kipsang alisema baadhi ya wazazi wanawapelekea watoto wao simu watakazotumia kuiba mtihani.

“Simu haziruhusiwi shuleni na hakuna mtihaniwa atakayeruhusiwa kuingia na simu katika chumba cha mtihani. Wazazi ndio wanaowapa simu au wanawatumia fedha za kununua simu.

“Wazazi watakaopatikana wakisaidia watahiniwa kupata simu watachukuliwa hatua za kisheria,” akaonya Dkt Kipsang.

Katibu wa wizara pia alifichua kuwa baadhi ya watahiniwa walio katika shule za mabweni wameanza kuzua ghasia ili waruhusiwe kufanya mtihani huku wakiwa nyumbani.

“Hiyo ni kazi bure kwani watahiniwa wote walio katika shule za bweni hawataruhusiwa kufanya mtihani wakitoka nyumbani. Watahiniwa wote waliojisajili katika shule za bweni watafanya mtihani wakiishi Kashuleni,” akasema.

Watahiniwa katika shule ambazo mabweni yake yaliteketezwa mwanzoni mwa mwaka huu watalazimika kulala katika vyumba vya madarasa hadi mtihani utakapokamilika mwezi ujao.

Dkt Kipsang pia alionya wanafunzi wanaotaka kutumia watu wengine kuwafanya mtihani kwa niaba yao akisema kuwa watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Wiki iliyopita, Dkt Kipsang, alionya kuwa watahiniwa wa kituo kitakachoripotiwa kuwa na kisa cha kutekeleza udanganyifu watazuiwa kuendelea na mtihani hivyo hawatapata matokeo yao.

Katibu huyo alisema wizara imetoa jumla ya Sh15 bilioni zitakazotumiwa katika maandalizi ya mtihani.

“Shule za upili zimepewa Sh12.5 bilioni na msingi Sh2.5 bilioni kwa ajili ya maandalizi ya mtihani,” akasema Dkt Kipsang.

Sehemu ya fedha hizo inatumika kununua kemikali ambazo hutumika kufanyia mitihani katika maabara.

Mwenyekiti wa Knec, Prof George Magoha alisema miongoni mwa shule zinazochunguzwa, nne ziko katika Kaunti ya Kisii, tano katika Kaunti ya Meru na tatu kaunti ya Garissa.

Mwenyekiti huyo juma lililopita, alisema kaunti nyingine zilizo na shule zinazochunguzwa ni Wajir, Pokot Magharibi na Kiambu.

Wawili hao walikuwa wakizungumza katika Taasisi ya Uundaji Mtaala (KICD) alipokutana na wawakilishi wa chama cha walimu wakuu wa shule za upili (Kessha) na msingi (Kepsha).

Mwaka jana, watahiniwa kutoka shule 10 za upili walikosa kupata matokeo yao kutokana na kuwepo kwa visa vya udanganyifu.

Watahiniwa 1,060,787 watafanya mtihani wa KCPE na 663,811 watafanya KCPE katika jumla ya vituo 10,075 kote nchini.

You can share this post!

Yaibuka Kibaki alitumia pesa za mlipa ushuru kufadhili...

Isaac Ruto amkosoa Raila kwa kushirikiana na Uhuru

adminleo