• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Wakulima wa majani chai kuvuna pesa za kihistoria

Wakulima wa majani chai kuvuna pesa za kihistoria

Na IRENE MUGO

WAKULIMA wa majani chai nchini wanajiandaa kupokea jumla ya Sh58 bilioni za bonasi kwa mazao waliyouza mwaka huu.

Hii itafikisha jumla ya pesa ambazo watakuwa wamelipwa mwaka huu hadi Sh86 bilioni, ambacho ndicho kiasi cha juu zaidi kuwahi kulipwa kwa wakulima wadogo wa majani chai katika historia ya kilimo hicho nchini.

Hili ni ongezeko ikilinganishwa na jumla ya Sh78 bilioni walizolipwa mwaka uliopita.

Ongezeko hilo la malipo ya jumla limefikia kiwango hicho licha kuwa bei ya kilo moja ya zao hilo imepungua hadi Sh52 ikilinganishwa na Sh58 mwaka jana.

“Hali hiyo imechangiwa na ongezeko la gharama za uzalishaji na kuzorota kwa bei,” akasema Bw Lerionka Tiampati, ambaye ndiye Afisa Mkuu wa Halmashauri ya Kusimamia Majani Chai (KTDA).

Licha ya kushuka kwa kiasi hicho, Bw Tiampati alisema wakulima watapokea Sh5 bilioni zaidi ikilinganishwa na mwaka uliopita kwani kulikuwa na ongezeko la mavuno ya majani chai.

“Mapato hayo yalichangiwa na kuongezeka kwa uzalishaji wa majani chai kwa asilimia 21 katika maeneo yanakokuzwa. Maeneo hayo yalipokea mvua kubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita, hali iliyochangia mavuno zaidi,” akasema Bw Tiampati.

Viwanda vyote vinavyosimamiwa na halmashauri hiyo vilipokea kilo 1.18 bilioni za majani chai, ikilinganishwa na kilo 976.78 milioni mwaka uliopita.

Wakulima wanatarajiwa kupokea fedha hizo za bonasi kufikia katikati ya mwezi huu.

Kila mwezi wakulima hao wapatao 600,000 hupokea Sh15 kwa kila kilo moja ya majani chai wanayouza. Hii imefanya kilimo hicho kuwa nafuu kuliko sekta nyingine kama vile kilimo cha kahawa, ambapo wakulima hulipwa mara moja pekee kwa mwaka,

Kaunti ambazo wakulima wanatarajiwa kunufaika na malipo hayo ya chai ni Kericho, Bomet, Kisii, Nandi, Nyeri, Kirinyaga, Kiambu, Murang’a, Embu na Meru.

You can share this post!

Mbunge akimbilia polisi baada ya kutwangwa na mkewe

Rais achemkia NCPB kwa kukosa kulipa wakulima

adminleo