• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Kura ya maamuzi kupunguzia Wakenya gharama ya maisha yaungwa mkono

Kura ya maamuzi kupunguzia Wakenya gharama ya maisha yaungwa mkono

BENSON MATHEKA Na SHABAN MAKOKHA

VIONGOZI mbalimbali wamesema kwamba wataunga kura ya maamuzi ambayo itawapunguzia Wakenya gharama ya maisha wala si kuongeza vyeo serikalini.

Walisema Wakenya wamelemewa na gharama ya maisha kutokana muundo wa serikali na kwamba hatua ya kuongeza vyeo kufaidi wanasiasa hakutasaidia umma.

Hayo yalijiri siku moja baada ya Naibu Rais William Ruto ambaye alikuwa amepinga kura hiyo kubadili nia na kukubali ifanyike.

Jana, kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi alisema kura ya maamuzi inafaa kulenga kuboresha maisha ya Wakenya na kuhakikisha kwamba hawataibiwa kura.

“Tulainishe Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) kwanza,” Bw Mudavadi alisema akiwa Kwale.

Nao viongozi wa eneo la Mlima Kenya walionya kuwa pendekezo la kufanyia Katiba mabadiliko linafaa kushughulikiwa kwa uangalifu ili lisiwagawanye Wakenya.

Walisema mabadiliko yoyote yanafaa kulenga kuimarisha maisha ya Wakenya kwa kutatua shida zao.

Wakiongea katika kanisa la St Nicholas AIPCA, Imenti ya Kati Kaunti ya Meru, viongozi hao walisema kwamba kura hiyo inaweza kutumia pesa nyingi lakini ikose kunufaisha Wakenya.

“Kura ya maamuzi ni kitu hatari. Huwa inagawanya jamii. Ghasia za baada ya uchaguzi mkuu za 2007/2008 zilichangiwa na kura ya maamuzi ya 2005,” alionya Gavana wa Kaunti ya Meru Kiraitu Murungi.

Naibu Rais William Ruto aliyehudhuria hafla hiyo hata hivyo alisisitiza kuwa kura hiyo haifai kuwa ya kubuni nyadhifa tofauti serikalini.

“Haifai kuwa ya kuunda viti tofauti. Inafaa kuwa ya kufaidi umma. Hii ndiyo sababu tunataka wale wanaoipigia debe waje tuketi kujadili kile kinachopaswa au kisichopaswa kuwa katika Katiba,” alisema Bw Ruto.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ya kuchanga pesa walikuwa wabunge Moses Kirima (Imenti ya Kati ), Rahim Dawood ( Imenti Kaskazini), Mpuri Aburi (Afrika Mashariki), Rindikiri Murwethania (Buuri) na Halima Mucheke (maalumu).

Wakiongea wakiwa Kakamega, wabunge Titus Khamala (Lurambi), Emmanuel Wangwe (Navakholo) na msaidizi wa Bw Ruto Faruk Kibet, walisema wataunga kura ya maamuzi ikiwa italenga kupunguza viti vya ubunge na kuondoa mgongano wa majukumu kati ya Serikali Kuu na serikali za Kaunti.

Walikuwa wakizungumza katika kanisa la Christ The King Catholic mjini Kakamega katika misa iliyohudhuriwa na aliyekuwa seneta wa Kaunti hiyo Boni Khalwale. Viongozi hao walisema kwamba kura ya maamuzi watakayounga mkono inafaa kuwa ya kupunguzia Wakenya mzigo wa kulipa ushuru.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya alisema ni makosa kwa baadhi ya viongozi kupinga mabadiliko ya Katiba kwa hofu ya kupoteza viti wanavyoshikilia kwa sasa.

Alisema kuwa wito wa kubadilisha Katiba umeshika kasi kwa sababu Wakenya wanakabiliwa na wakati mgumu kiuchumi. Alisisitiza kwamba kura ya maamuzi inafaa kuwa ya kuboresha maisha ya Wakenya.

You can share this post!

Tabasamu kwa wanafunzi Helb ikitoa Sh13.7b kufadhili masomo

Mbuga ya Maasai Mara bado namba wani Afrika

adminleo