• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Anaswa na sanduku lake la aiskrimu alilosafirishia bangi

Anaswa na sanduku lake la aiskrimu alilosafirishia bangi

Na CHARLES LWANGA

MKUU wa Polisi Kaunti ya Kilifi amewataka maafisa wa polisi kuwa makini katika vita dhidi ya mihadarati baada ya walanguzi kuvumbua mbinu mpya kusafirisha dawa hizo bila kujulikana.

Kamanda wa polisi wa Kaunti hiyo, Bw Fredrick Ochieng’, alitoa ushauri huo baada ya kunasa misokoto 160 ya bangi zenye thamani ya Sh32,000 zilizokuwa zinasafirishwa kwenye sanduku la aiskrimu.

“Bangi hizo zilikuwa zinasafirishwa kwa pikipiki kutoka Maweni huko Malindi kuelekea Mamburui kabla ya kushikwa na maafisa wa polisi maeneo ya Sabaki kwenye Barabara Kuu ya Malindi-Lamu,” alisema.

Bw Ochieng’ alisema mshukiwa, Bw Muhamed Salim, mwenye umri wa miaka 25 alishikwa na kufikishwa kwenye kituo cha polisi cha Malindi kwa mahoji zaidi.

“Mshukiwa atafikishwa kortini na kushtakiwa. Tutabadilisha mbinu zetu za kupambana na mihadarati ili tuhakikishe hakuna mbinu inayotumiwa kuingiza na kusafirisha mihadarati Kilifi,” akasema.

Mara nyingi, wakazi wamekuwa wakidai kuwa waendeshaji bodaboda wamekuwa wakitumiwa kusafirisha mihadarati na pia kusafirisha wahalifu.

Haya yanajiri wiki chache baada ya majasusi kushika bangi kilo 100 zenye thamani ya Sh300 milioni huko Kikambala zilizokuwa zimefichwa kwenye mkoba wa nguo.

Polisi bado wanamsaka mwanamke anayemiliki nyumba hiyo anayedaiwa kutoroka kabla ya maafisa hao kufika nyumbani kwake.

Mwezi uliyopita, shirika la kijamii la kupambana na mihararati mjini Malindi-Omar Project lilisema takriban vijana 300 huwacha masomo kila mwaka kutokana na mihadarati.

Bw Edison Mwabonga, ambaye ni afisa wa miradi katika shirika hilo alisema vijana 900 wenye umri wa miaka 18 hadi 37 walioathiriwa na mihadarati wanapokea matibabu ya ‘Methadone’ katika hospitali ya Malindi.

You can share this post!

Wahisani waagizwa kutii kanuni za KCPE wakitoa mlo

Joho aanzisha mikakati ya kuzima waasi katika ODM

adminleo