• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
ROBERTO FIRMINO: Chuma thabiti na injini imara ya Liverpool

ROBERTO FIRMINO: Chuma thabiti na injini imara ya Liverpool

Na CHRIS ADUNGO

ROBERTO Firmino Barbosa de Oliveira, 27, ni fowadi matata mzawa wa Brazil ambaye kwa sasa anainukia kuwa miongoni mwa nyota wa kutajika chini ya ukufunzi wa Jurgen Klopp kambini mwa Liverpool. Baada ya kujitosa katika taaluma ya usakataji kabumbu akivalia jezi za Figueirense mnamo 2009, Firmino alisajiliwa baadaye na Hoffeinheim kwa mkataba wa miaka minne na nusu.

Mabao 16 aliyowafungia miamba hao wa soka ya Ujerumani katika mechi 33 za Bundesliga yalimwezesha kutia kapuni taji la Mchezaji Bora wa msimu wa 2013-14.

Mnamo Julai 2015, Firmino alitua nchini Uingereza kuvalia jezi za Liverpool uwanjani Anfield. Ubunifu wake, wepesi wa kufunga mabao na ujuzi wa kuwapiga chenga wapinzani; ni sifa ambazo zimemweka miongoni mwa wachezaji wanaostahiwa pakubwa ndani na nje ya bara Ulaya.

Mwishoni mwa msimu jana, Klopp aliungama kuwa Firmino ni injini ya Liverpool kila mara kikosi hicho kinapoamua kutandaza soka ya kushambulia.

Firmino aliwajibishwa ndani ya jezi za timu ya taifa ya Brazil kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 2014 na alikuwa tegemeo kubwa katika fainali za Copa America mnamo 2015 na Kombe la Dunia 2018.

Akiwa mzawa wa eneo la Maceio viungani mwa mji wa Alagoas, Firmino alianza kupiga soka katika academia ya Figueirense mnamo 2008 akiwa kitoto cha miaka 17 pekee. Awali, alikuwa amewasakatia Club de Regatas Brasil (CRB) ambapo kipaji chake kilitambuliwa na Marcellus Portella aliyemwajibisha pakubwa kama beki mkabaji.

Kibarua chake cha kwanza ndani ya kikosi cha Figueirense ni mchuano uliowakutanisha na Ponte Preta na kumalizika kwa wao kupoteza 1-2. Ilikuwa hadi Januari 2010 ambapo Firmino alipandishwa daraja kuunga kikosi cha kwanza cha Figueirense Toninho.

Firmino alipachika wavuni bao lake la kwanza ndani ya kikosi cha waajiri wake hao mnamo Mei 8, 2010 katika mechi iliyowakutanisha na Sao Caetano. Katika msimu huo wa 2009-10, Firmino aliwafungia Figueirense jumla ya mabao manane katika michuano 36 na hivyo kuwachochea kurejea kwenye kivumbi cha Ligi Kuu ya Serie A baada ya kukaa nje kwa kipindi cha miaka miwili.

Mnamo Desemba 2010, Firmino alitia saini mkataba wa miaka minne na nusu na Hoffeinheim walioanza kujivunia huduma zake mwanzoni mwa Januari 2011.

Mechi yake ya kwanza ni kibarua kilichowakutanisha na Mainz katika mechi ya Bundesliga. Katika mchuano huo, Firmino alitokea benchi katika dakika ya 75 kujaza pengo la Sebastian Rudy.

Bao la kwanza la Firmino ndani ya jezi ya Hoffenheim ni mchuano uliowakutanisha na Eintracht Frankfurt mnamo Aprili 16, 2011.

Kwa pamoja na Chinedu Obasi, walitemwa kwenye kikosi cha kwanza cha waajiri wao mnamo Novemba 2011 baada ya kuanza kuchelewa kufika kambini pa mazoezi.

Baada ya kosa hilo kumweka nje ya mechi iliyowakutanisha na Bayer Levekusen, Firmino alifunga mabao mawili zaidi dhidi yay a Wolfsburg na Borussia Monchengladbach. Katika msimu wa 2012-13, aliwajibishwa katika michuano 36 na kupachika wavuni mabao saba.

Mnamo Julai 2013, kikosi cha Lokomotiv Moscow nchini Urusi kilianza kuyahemea maarifa ya Firmino kwa kima cha Sh1.4 bilioni. Hata hivyo, aliyekuwa nahodha wa Hoffenheim, Andreas Beck alimshawishi Firmino kutoagana na waajiri wake na badala yake, fowadi huyo akarefusha muda wa kuhudumu kwake nchini Ujerumani kwa kutia saini mkataba mpya wa miaka mitatu.

Kuimarika kwa makali yake katika msimu wa 2013-14 kulimfanya kuwa miongoni mwa wanasoka wanne waliotawala orodha ya wafungaji bora wa Bundesliga. Alitikisa nyavu za wapinzani mara 16 na kutawazwa Mchezaji Bora wa msimu huo.

Mnamo Juni 23, 2015, Firmino aliagana na Hoffenheim baada ya Liverpool kuziwania huduma zake wakati akiichezea Brazil katika fainali za Copa America. Mwishoni mwa kivumbi hicho kilichotawaliwa na Chile, Firmino aliingia katika sajili rasmi ya Liverpool baada ya kupata kibali cha kufanyia kazi nchini Uingereza mnamo Julai 4.

Kibarua chake cha kwanza uwanjani Anfield ni mchuano wa kirafiki uliowakutanisha na Swindon Town mnamo Agosti 2, 2016. Alitokea benchi kunako dakika ya 78 kujaza nafasi ya Jordon Ibe mnamo Agosti 9 katika ushindi wa 1-0 waliousajili dhidi ya Stoke City katika mechi ya EPL.

Alifungua rasmi akaunti yake ya mabao kambini mwa Liverpool mnamo Novemba 21 alipowachochea waajiri wake kuwapepeta Manchester City 4-1 uwanjani Etihad. Hata hivyo, ushirikiano kati yake na fowadi wa zamani wa Aston Villa, Christian Benteke haukuzalisha mabao mengi jinsi ilivyotarajiwa na mashabiki wa miamba hao wa soka ya Uingereza.

Ilikuwa hadi mwanzoni mwa 2016 ambapo fomu ya Firmino ilianza kuimarika chini ya Klopp aliyemchezesha mara nyingi kama mvamizi mkuu. Alifunga mabao manne dhidi ya Arsenal na Norwich City katika tukio lililomvunia taji la Mchezaji Bora wa Mwezi Februari na hivyo kuwafanya wadadisi wa soka kuanza kulinganisha upekee wa uwezo wake na ule wa Raheem Sterling. Alikamilisha kampeni za msimu huo akijivunia jumla ya mabao 10 kibindoni.

Uwepo wa Firmino, Mohamed Salah na Sadio Mane kambini mwa Liverpool ni jambo ambalo kwa sasa linafanya timu hiyo ya Klopp kuwa miongoni mwa vikosi vinavyojivunia mafowadi bora zaidi katika soka ya bara Ulaya.

Frimino alifunga pingu za maisha na kichuna Larissa Pereira mnamo Juni 2017; na wamejaliwa watoto wawili wa kike.

You can share this post!

OBARA: Kaunti ya Mombasa inakosea kupuuza wawekezaji wadogo

MOKAYA: Mourinho ni kuku wa kuchinjwa

adminleo