• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
TAHARIRI: Sikukuu ziwe zenye manufaa kwa taifa

TAHARIRI: Sikukuu ziwe zenye manufaa kwa taifa

NA MHARIRI

WAKENYA wengi Oktoba 10, 2018 wameamka wakiwa hawana mipango ya kwenda kazini, baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kutangaza Jumatano kuwa Sikukuu mnamo Jumatatu.

Katika kuitaja siku ya Oktoba 10 kuwa Sikukuu, waziri huyo hakuwa na maelezo ya ziada kuhusu kinachoadhimishwa wala mipango yoyote ya kuiadhimisha.

Siku kama ya leo ilikuwa ikiadhimishwa kwa jina la Moi Dei, kukumbuka Rais wa pili wa Kenya, Mzee Daniel Toroitich arap Moi alipoingia mamlakani. Lakini Wakenya walipoidhinisha katiba Mpya Oktoba 2010, Moi Dei haikuwa mojawapo ya siku hizo. Hata ile iliyojulikana kama Kenyatta Dei iligeuzwa jina na kuwa Sikukuu ya Mashujaa.

Mojawapo ya sababu ilikuwa kwamba sikukuu hiyo haikuwa ya kuadhimisha wananchi au ufanisi wa nchi, bali mtu mmoja. Lakini pia, siku chache kabla ya kuondoka mamlakani, Mzee Moi mwenyewe alikuwa amependekeza kuwa iwe ikiadhimishwa kwa kuwajali wasiobahatika katika jamii na wala si kwa sherehe kama sikukuu nyingine za kitaifa.

Kwa hivyo, Jaji George Odunga alipoamua mwaka 2017 kwamba Moi Dei yafaa kuwa sikukuu, hakuna aliyezingatia kuwa tungeiadhimisha tena leo.

Sikukuu hii haimo kwenye orodha ya zile sikukuu za kitaifa. Inaeleweka kuwa hata mojawapo ya sikukuu za Idd (Eid-Ul-Fitri) haiko kwenye katiba. Tofauti ya Idd na Moi Dei ni kuwa moja inawahusisha watu wengi.

Kenya sasa hivi inapitia kipindi kigumu cha uchumi na wananchi wanahitaji kujifunga vibwebwe zaidi kufanya kazi kwa bidii. Takwimu za majuzi kuhusu uchumi zinaonyesha umeporomoka ikilinganishwa na ulivyokuwa mwaka jana.

Rais mstaafu Mwai Kibaki alikuwa daima akihimiza kuwa watu wafanye kazi. Alifahamu kwamba nchi yoyote ulimwenguni haiwezi kupiga hatua ikiwa watu wake watakuwa wa kusherehekea kila mara bila ya kuwa na ufanisi wowote.

Katika mataifa kama vile Japan na Korea Kusini, serikali huwalazimisha raia wake kuchukua likizo. Watu wa mataifa hayo ni wachapa kazi ambapo baadhi hulala na kuamkia kazini. Matokeo yake ni kutokea kwa miundo mipya ya magari na vifaa vya kielektroniki karibu kila siku.

Je, sisi Kenya ambao hatuna hata kiwanda cha kuunda baiskeli, tunahitaji sikukuu zaidi ya 12 kwa mwaka za kufanyia nini?

You can share this post!

MOI DEI YA MAUTI: Watu 55 waangamia ajalini

Kioja pasta kusaka tiba kwa mganga

adminleo