• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
Makanisa yataka serikali izime ‘Samantha’

Makanisa yataka serikali izime ‘Samantha’

Kinyago cha wanaume kujiburudisha kimapenzi almaarufu ‘Samantha’. Makanisa yameitaka serikali kuzima biashara hii. Picha/ Hisani

 

Na MWANGI MUIRURI

Kwa muhtasari:

  • Askofu Hillary Mugo aitaka serikali kukomesha biashara ya ‘Samantha’
  • Makanisa yamtaka waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i ajumuishe misako dhidi ya vinyago hivyo
  • Tamadauni za kizungu zakataliwa nchini

MUUNGANO wa Wakristo ukanda wa Mlima Kenya, unaitaka serikali iunde sheria ya kupiga marufuku utumizi wa vinyago vya mahaba hapa nchini, hasa muundo wa ‘Samantha’.

Unasema utumizi wa vinyago hivyo ni upotovu wa kimaadili na hali inayoashiria uabudu wa shetani.

Mwenyekiti wao, Askofu Hillary Mugo, muungano huo ulisema Jumamosi kwamba serikali hadi sasa inaonekana kuchukulia mwelekeo huo wa kuunda vinyago hivyo na kuvisambaza mashinani kama njia moja ya kibiashara.

Akiongea Mjini Murang’a, askofu huyo alisema kuwa hadi sasa vinyago hivyo vimepenya mashinani na ambapo majumba spesheli ya kuburudika mahaba yanapokea wateja wa kushiriki mahaba kwa malipo na vinyago hivyo.

“Niko na ushahidi kuwa katika mitaa ya Githunguri katika Kaunti ya Kiambu, Nyeri, Murang’a na Kirinyaga kuna ‘Samantha’ hao. Wazee kwa vijana wanajumuika kulipa ada ili washiriki mahaba na hilo ni suala la kishetani,” akateta.

Alisema kuwa serikali isiyowajibikia masuala ya kimaadili na kuwahimiza watu wake wafuate mkondo uliowekwa na tamaduni za kijamii na maandiko matakatifu kuhusu ndoa na mahaba ni mshirika wa ushetani.

‘Uzungu’

“Tulianza na kuletewa ‘Uzungu’ wa ndoa za jinsia moja pamoja na biashara ya ukahaba ndani ya mpangilio huo potovu. Tukawa na vinyago vya kuridhisha wanawake kimahaba na tena tukawa na watoto wetu wa kike wakisajiliwa katika mitandao ya biashara ya ngono na wanyama. Sasa tumeletewa Samantha na serikali haijaongea kupinga kwa kuwa hatutarajii iunge mkono,” akasema.

Askofu Mugo alimtaka waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i ajumuishe misako dhidi ya vinyago hivyo sambamba na magenge haramu na pia mitambo ya kamari katika amri zake za misako.

Aidha, ameitaka serikali izindue mpango maalum wa kutoa imani ya kimaisha kwa vijana wa taifa hili “ambao wameishiwa na uvumilivu dhidi ya mahangaiko ya kimaisha kiasi kwamba kujituliza, badala ya wakimbizane na ya kuwafaa maishani, wanafuatana na yale ya kuwaangamiza.”

Alisema kuwa misukosuko ndani ya ndoa inhayoshuhudiwa kwa sasa imetokana na kuishiwa na imani hiyo kwa maisha kiasi kwamba “sasa kuepuka mahangaiko, kuna mauaji, ulevi kiholela, utumizi wa mihadarati na sasa kujituliza hisia za mahaba na vinyago.”

You can share this post!

Mawakili kugoma kulalamikia mazoea ya serikali kukaidi...

Simanzi katika hafla ya waliokufa katika ajali ya ndege

adminleo