• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
MOI DEI: Mbinu alizotumia Mzee Moi kuteka hisia za Wakenya

MOI DEI: Mbinu alizotumia Mzee Moi kuteka hisia za Wakenya

Na CHARLES WASONGA

KATIKA miaka 24 akiwa mamlakani Rais Mstaafu Daniel Arap Moi alikuwa akisikika na kila Mkenya kwa sababu habari zake zilikuwa zikipeperushwa kila mara redioni na kwenye runinga.

Na nyakati ambapo hakuwa na shughuli rasmi katika ratiba yake, Mzee Moi angejitokeza mitaani au katika barabara za miji mikuu kununua mahindi choma, na matunda, angalau kudhihirishia umma kuhusu uwepo wake.

Nyakati za wikiendi angehudhuria mikutano ya kuchangisha pesa, harusi au mazishi ya watu mashuhuri, shughuli ambayo zingeangaziwa katika vyombo vya habari.

Na siku za Jumapili, ilikuwa ada kwa Rais mstaafu Moi kujumuika na wanafunzi na walimu wa Shule ya Upili ya Moi Kabarak kwa ibada ya Jumapili. Kando na hapo alipenda kuhudhuria ibada katika Kanisa la AIC, eneo la Milimani, Nairobi.

Hii ndio maana taharuki ilitanda nchini na mataifa ya nje, Mzee Moi alipokosa kuonekana hadharani wala kusikika kupitia vyombo vya habari kwa muda wa wiki moja mwishoni mwa Januari, 1995.

Hata viongozi wa upinzani waliokuwa na mazoezi ya kushambulia serikali ya Mzee kila mara waliingiwa na wasiwasi, hali iliyopelekea baadhi yao kuitisha kikao na wanahabari wakitaka taarifa kutoka kwa serikali kuhusu aliko kiongozi wa taifa.

Uvumi ulianza kuenea kwamba Mzee Moi alikuwa anaugua, hali ambayo iliibua kiwewe humu nchini na katika jamii ya kitaifa.

Hii ni kwa sababu uthabiti ulihitajika nchini, ili kuwezesha mataifa ya kigeni kupambana na utovu wa usalama katika mataifa jirani ya Somalia, Sudan Kusini na Rwanda.

Ni wakati huo ambapo wanasiasa vijana enzi hizo; Kiraitu Murungi (sasa Gavana wa Meru), Kivutha Kibwana(Makueni), Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Mukhisa Kituyi na Paul Muite ambao walikuwa wanachama wa vuguvugu la Mwangaza Trust walipanga kubuni muungano wa kumwondoa Moi mamlakani.

Mashirika kadhaa yaliyokuwa yakifadhiliwa na Amerika na Ujerumani pia yaliunga mkono juhudi hizo.

Wiki hiyo na “kupotea” kwa Moi ilikamilika kwa kishindo baada ya kiongozi huyo kujitokeza jijini Nairobi.

“Huku akitabasamu alisimama nje ya afisi yake katika jumba la Harambee akisema: “Je, naonekana mtu mgonjwa? Je, naonekana kama mtu alirejea kutoka ulimwengu wa wafu?

Umati wa watu ulikusanyika nje ya afisi hizo huku wakimshangilia.

Hivyo ndivyo Mzee Moi alithibitisha kuwa ni rais aliyethibiti hisia za wananchi wote licha ya shtuma kutoka kwa viongozi wa upinzani na jamii za kimataifa.

Wakati huo huo, Rais mstaafu pia anakumbukwa kwa juhudi zake katika uhifadhi wa mazingira na kupambana na mmomonyoko wa udongo.

Siku moja mnamo Machi 1982, alipeleka kampeni hizo wilayani Machakos ambapo ilimlazimu kuendesha mkutano wa baraza lake la mawaziri chini ya mti kabla ya kuongoza shughuli ya kujenga miundo mbinu ya kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Hiyo ndiko ilikuwa kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri kuendeshwa eneo wazi nje ya Ikulu ya Nairobi au afisi ya Rais katika Jumba la Harambee.

Mawaziri hawakuvalia suti kwani hata aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kikatiba Charles Njonjo, kwa mara ya kwanza maishani mwake, alionekana amevalia long’i ya jeans na fulana.

You can share this post!

IEBC ilipoteza Sh9.5b katika uchaguzi 2017 – Ripoti

Mwalimu Thomas Wasonga alivyomchangamsha Moi kwa utunzi wa...

adminleo