• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Wabunge na maseneta wamtaka Uhuru kumwadhibu Boinnet kuhusu ajali ya Kericho

Wabunge na maseneta wamtaka Uhuru kumwadhibu Boinnet kuhusu ajali ya Kericho

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE na Maseneta wameungana kulaani ajali ya iliyohusisha basi moja la abiria lilitokea katika eneo la Fort Ternan, kaunti ya Kericho na kusababisha vifo vya watu 58 huku wengine 13 wakijeruhiwa.

Wanachama wa mabunge hayo mawili walitenga fursa maalum katika vikao vya alasiri kutoa rambirambi zao kwa familia na marafiki ya waathiriwa wa ajali hiyo iliyotokea Jumatano alfajiri.

Basi hilo kwa jina Home Boyz lilikuwa likisafiri kutoka Nairobi kwenda Kakamega ajali hiyo ilipotokea baada ya dereva kushindwa kulidhibiti na ndipo likabingiria mara kadhaa.

Wabunge hao na maseneta walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwawajibisha mawaziri James Macharia (Uchukuzi), Fred Matiang’i (Usalama) na ajali hiyo ambayo ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini.

Vile vile, walimtaka kiongozi wa taifa kumwadhibu Inspekta Jenerali Joseph Boinnet kufuatia ajali hiyo.

Viongozi hao walisema ajali katika barabara zetu zinaweza kuzuiwa lakini wakalumu asasi husika na kuhakikisha kuwa sheria za trafiki zinazingatiwa ndio zimezembea katika majukumu yao.

“Shida kuu ni ufisadi ambao umekithiri katika barabara zetu. Jinamizi hili linafaa kupigwa vita kupitia adhabu kali kwa wahusika,” akasema kiongozi wa wachache katika seneti Bw James Orengo.

“Mashirika ya serikali yanayosimamia usalama barabarani ndiyo yamezembea kazini huku akipendekeza Dkt Matiang’i na Boinnet wachukuliwe hatua,” akasema Seneta huyo wa Siaya akichangia hoja ya kujadili mkasa huo baada seneti kusitisha shughuli zake rasmi.

“Rais anafaa kuhakikisha maafisa hawa wanawajibikia ajali hiyo. Sharti wafutwe kazi ili iwe mfano kwa maafisa wa ngazi za chini katika asasi za serikali wanazoongoza,” akasema Bw Orengo huku akiungwa mkono na seneta wa Nairobi Johnson Sakaja.

Na katika Bunge la Kitaifa Mbunge Mwakilishi wa Busia Florence Mutua alisema ni aibu kwa taifa hili kuendelea kupoteza watu katika barabara zake ilhali kuna asasi ambazo zimepewa majukumu ya kudumisha usalama.

“Hii sekta ya uchukuzi imekosa usimamizi bora. Hali ilikuwa tofauti wakati marehemu John Michuki alisimamia wizara hii ya uchukuzi,” akasema Bi Mutua ambaye alianzisha hoja ya kuitaka bunge kujadili ajali hiyo.

Mbunge Maalum Bi Denitah Ghati ambaye ni mwathiriwa wa ajali aliilaani wizara ya uchukuzi kwa kushindwa kuimarisha usalama barabarani ilhali asasi zake zinafadhiliwa kwa fedha za umma.

“Kenya haikabiliwi na uhaba wa sheria za kuzuia ajali za barabarani. Shida ni uzembe wa maafisa waliotwikwa jukumu la kuhakikisha kuwa sheria hizo zinazingatiwa na kutekelezwa. Wanafaa kufutwa kazi mara moja,” akasema Bi Ghati ambaye hutumia kiti cha magurudumu baada ya kuhusika katika ajali katika barabara ya Narok kwenda Kisii miaka minne iliyopita.

You can share this post!

AJALI BARABARANI: Kiini cha watu kuzidi kuangamia Kenya

Haji amwamuru Boinnet achunguze ajali ya Fort Ternan

adminleo