• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
Waziri Mkuu awafanyisha wanajeshi mazoezi kuzima maandamano

Waziri Mkuu awafanyisha wanajeshi mazoezi kuzima maandamano

Na PETER MBURU

WAZIRI Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitumia akili ya hali ya juu wakati wanajeshi wa nchi hiyo walisusia kazi na kuandamana hadi afisini mwake wakiwa na silaha, alipowaambia wafanye mazoezi ya ‘press ups’ kwa pamoja, ili kujichangamsha.

Bw Ahmed ambaye alionyesha kutoridhishwa na hatua ya wanajeshi hao waliofika katika makao yake wakidai kuongezewa mshahara aliwaomba wafanye ‘press-ups’ kumi, ili kutuliza hali kwanza.

Mamia ya walinda usalama hao walikuwa wamesababisha wasiwasi kuhusu usalama wa kiongozi huyo, hali hiyo ikisababisha kufungwa kwa mabarabara na intaneti kufungwa saa kadhaa.

Lakini weledi wa kiongozi huyo uliyeyusha hasira ya wanajeshi hao kwani walipokuwa wakifanya mazoezi hayo walijawa na tabasamu, ishara kuwa suluhu ilikuwa imepatikana kwa Amani.

Wanajeshi hao walikuwa wameanza kuandamana Jumatano asubuhi, hali iliyosababisha baadhi ya barabara kufungwa. Baadaye alasiri, waliruhusiwa kuingia makazi ya Rais baada ya kuwacha silaha nje.

Wachanganuzi nchi hiyo walieleza kuwa hali ya mgomo huo kuandaliwa hadi kutekelezwa bila ya idara za ujasusi kufahamu lolote ilidhihirisha utepetevu wa usalama nchini humo.

Mwanajeshi wa zamani alieleza BBC kuwa malalamiko ya wanajeshi hao yalikuwa ya haki, lakini akasema mbinu walizotumia zilikiuka utaratibu na adabu za kijeshi.

“Hii inaashiria kuwa vifaa vya kijeshi na kijasusi haviko tayari kumhudumia kiongozi mpya wa serikali na mageuzi anayoleta,” akasema mtaalam wa sheria Dereje Zeleke.

Waziri Mkuu huyo ameleta mageuzi mengi tangu alipoingia katika serikali.

Baada ya kukutana na wanajeshi hao, Bw Abiy aliahidi kuyaangazia malalamiko yao, japo akasisitiza kuwa hata wafanyakazi wa serikali wanafaa kuridhika na mshahara mdogo wanaolipwa kwa kuwa serikali hiyo haina pesa za kutosha.

“Tunafaa kutumia pesa kwa miradi ya maendeleo. Tunaweza kumlipa kila mtu mshahara mkubwa lakini tutabaki bila maendeleo,” akasema kupitia ujumbe.

Kiongozi huyo aliingia afisini mnamo Aprili na amekuwa akifanya juhudi kutafuta Amani ndani nan je ya nchi yake.

You can share this post!

Haji amwamuru Boinnet achunguze ajali ya Fort Ternan

OBADO ANYONGWE – DPP

adminleo