• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:40 AM
Matiang’i aapa kuwanyaka wezi wote wa mitihani

Matiang’i aapa kuwanyaka wezi wote wa mitihani

Na VALENTINE OBARA

WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, ameahidi kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa mitihani ya kitaifa ya mwaka huu ili kuzuia wizi sawa na jinsi alivyokuwa akifanya alipokuwa Waziri wa Elimu.

Waziri huyo jana alifichua mipango mipya ambayo wizara yake inatazamia kutekeleza ili kukabiliana na yeyote atakayejaribu kuhadaa wanafunzi kuiba mitihani hiyo itakayoanza wiki ijayo.

Kulingana na Dkt Matiang’i, mwaka huu kutakuwa na ushirikiano wa karibu kati yake pamoja na Inspeta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kuzuia wizi wa mitihani.

Mabw Haji na Kinoti wamejizolea sifa nchini kwa jinsi wanavyopambana na aina tofauti za uhalifu, hivyo basi kushiriki kwao mapema katika usimamizi wa mitihani ni hatua muhimu.

“Sina shughuli nyingine yoyote kuanzia Oktoba 29. Nitakuwa nanyi kufungua kontena za mitihani asubuhi na mapema. Sijawahi kutatizika kurauka wala kusafiri maeneo ya mbali nchini,” akasema.

Kwa wanaopanga kuiba mitihani hiyo, alionya: “Hatutakuwa na huruma. Tuna jukumu kusaidia watoto wetu kuendeleza mbele elimu yao,” akasema.

Akizungumza katika mkutano wa manaibu makamishna wa kaunti na maafisa wa elimu kwa maandalizi ya mitihani hiyo jijini Nairobi, aliongeza kuwa wanafunzi huwa wamejitayarisha vyema lakini watu wazima, wakiwemo wazazi na walimu ndio hutaka kuwapotosha kwa kuwatia hofu mitihani inapokaribia.

Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) umepangwa kuanza Jumatatu ijayo na watahiniwa 664,586 wamejisajili, huku ule wa shule za msingi (KCPE) ulio na watahiniwa 964,119 ukitarajiwa kuanza Oktoba 30.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na maafisa wa Wizara ya Elimu wakiongozwa na Waziri Amina Mohamed na Katibu wa Wizara Belio Kipsang.

Dkt Matiang’i na Bi Mohamed walitangaza kuwa maafisa wa wizara zao hawataruhusiwa kuenda likizoni hadi mitihani ya kitaifa itakapokamilika.

“Tumetuma kote nchini maafisa wa kutosha wa usalama. Ninawahakikishia kuwa watoto katika kila eneo watafanya mitihani yao bila tatizo,” akasema.

Bi Mohamed alikariri mipango iliyowekwa na wizara yake kuzuia wizi wa mitihani mwaka huu, na kusema kontena 459 za kuhifadhi mitihani katika kaunti ndogo za nchi zitafungwa kwa vifuli viwili.

Funguo zitakuwa mikononi mwa Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti Ndogo na Naibu Kamishna wa Kaunti pekee, ambao itakuwa lazima wafungue na kufunga kontena hizo wakiwa pamoja.

“Ninamhakikishia Dkt Matiang’i kwamba msingi alioweka miaka miwili aliyokuwa katika wizara ya elimu iko imara na ujenzi tunaofanyia msingi huo pia utakuwa imara,” akasema.

Mwaka huu karatasi za mitihani inayofanywa asubuhi hazitaruhusiwa kuondolewa katika vyumba vya mitihani hadi mitihani yote ya siku hiyo ikamilike. Bi Mohamed alisema hatua hii inalenga kuzuia karatasi hizo kufanyiwa mabadiliko.

You can share this post!

Ibada ya wafu ya walioangamia ajalini kufanyika Jumatano

Mungatana akiri kupoteza hela lakini sio kwa waganga

adminleo