• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Wachezaji wa humu nchini na majuu ni sawa, Migne asema

Wachezaji wa humu nchini na majuu ni sawa, Migne asema

Na CECIL ODONGO

KOCHA Mkuu wa timu ya taifa, Harambee Stars Sebastien Migne anaamini kwamba wachezaji wanaosakata soka nyumbani wana umuhimu mkubwa kama tu wenzao wanaowajibikia gozi la kulipwa katika mataifa nje haswa mashindano ya AFCON 2019 yakizingatiwa.

Ili kushadidia kauli hiyo, mkufunzi huyo raia wa Ufaransa alimsifia kiungo mbunifu Dennis Odhiambo ambaye amekuwa mhimili mkubwa kwenye kikosi cha Stars katika kampeni yao ya kufuzu Kombe la Bara Afrika mwaka ujao.

“Kila mchezaji hutoa mchango aula kwa timu ndiyo maana tunafaa kupuuza dhana potovu kwamba wale wanaopiga soka nje ya nchi wapo katika kiwango cha juu kuliko wenzao wa KPL. Kile muhumi sana ni uwajibikaji na kujituma. Mfano maridhawa ni Dennis Odhiambo ambaye amepigia Stars soka safi na kuchangia ufanisi wetu,” akasema Migne.

Mwanadimba huyo wa Sofapaka amezua ushirikiano wa kupigiwa mfano na nahodha wa timu ambaye pia husakatia Tottenham Hot Spurs Victor Wanyama na vile vile kummegea pasi safi mshambulizi Ismael Gonzalez katika mechi zilizopita za Stars.

Aidha Migne alifichua kwamba analenga kuzua ushirikiano mkubwa na wachezaji wa ligi ya nyumbani kabla msimu mpya wa KPL kung’oa nanga mwezi Disemba.

“KPL kwa sasa iko mapumzikoni lakini tutaendelea na kazi. Natumai nitafikia makubaliano ya kupanga ratiba kwa wachezaji wa timu ya taifa wanaosakata soka nyumbani ili tuwe tukishiriki mazoezi kwa saa chache mara nyingi kwa wiki. Ila kilichomuhimu ni wao kupumzika kwanza wakisubiri msimu uanze,’ akaongeza Migne.

Harambee Stars itakwaruzana na Sierra Leone katika mechi yao ijayo iwapo Shirikisho la soka duniani, FIFA itafutilie mbali marufuku iliyowekewa taifa hilo na Shirikisho la Bara Afrika CAF, iliyoiondoa katika mashindano hayo baada ya serikali yake kuingilia maswala ya soka kinyume na sheria za FIFA.

You can share this post!

Juve ilinifukuza ili kupisha Ronaldo – Higuain

Ushahidi dhidi ya mganga wa Kangundo wakosekana, aachiliwa...

adminleo