• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
WAMALWA: Tuutumieni uvumbuzi wa kiteknolojia kuimarisha usomaji wetu

WAMALWA: Tuutumieni uvumbuzi wa kiteknolojia kuimarisha usomaji wetu

NA STEPHEN WAMALWA

MWANZONI mwa Oktoba, nilifanya tathmini ya usomaji wetu wa vitabu katika maisha ya kila siku.

Wengi wetu tunakiri kuwa, licha ya kuwa taifa mojawapo lililo na idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika barani Afrika, bado hatujajitendea haki katika kuutilia maanani usomaji wa vitabu.

Baadhi ya wasomaji wa makala haya mitandaoni wanasema kuwa, ni vigumu sana kushika kitabu mkononi kusoma kwa kuwa yapo mengi ya dharura maishani yanayofaa kushughulikiwa.

Kauli zao zina ukweli japo mdogo hasa ukilinganisha kuwa, sisi tu taifa lililo mbioni kila uchao kutafuta riziki na kujenga hali zetu za leo na kesho. Ila niliwahi kujiuliza na sasa ninauliza tena, je, umewahi kutathmini shughuli zako kwa muda wa saa ishirini na nne unazojaliwa na Mungu duniani kila siku?

Je, mbali na shughuli zako za kila siku za kujitafutia riziki na mengine mengi ya kibinafsi, unatumia muda upi kuwa mtandaoni? Unapokuwa kwenye mtandao, wewe husakura mambo yepi? Je, umewahi kuyaona majarida, makala au vitabu mtandaoni ambavyo unaweza kupakuwa bure bila malipo?

Bila shaka yapo makala, majarida na vitabu vizuri sana mtandaoni labda katika mfumo wa PDF (Portable Document Format). Hazina hii haihitaji ulipie gharama za usafiri au za ununuzi.

Teknolojia imetuwezesha kuufumbata ulimwengu na hekima zake katika viganja vyetu. Wasomi wa teknolojia habari na mawasiliano wanasema kuwa ishara muhimu ya utandawazi ni ule uwezo wake wa kuyagusa maisha ya wanajamii wengi kwenye jamii anuwai katika nyanja za elimu, uchumi, siasa na utamaduni kwa jumla.

Teknolojia ya mtandao imetuwezesha kufikia hazina hizi kwa wepesi mno kokote tuliko kwa wakati wowote almradi umeunganishwa kwenye masafa ya mtandao.

Yaani unaweza ukavinjari tovuti mbalimbali za vyombo vya habari, mashirika yanayochapisha makala na vitabu pamoja na tovuti za watu na mashirika binafsi na kupakua hazina hii.

Mitandao kama vile facebook, Wechat na WhatsApp miongoni mwa nyingine inatuwezesha kuunda kumbi. Kumbi hizi zinaweza kutusaidia kuhamasishana kusoma vitabu mbalimbali.

Labda baada ya kuvisoma vitabu hivyo, tunaweza kuvichambua kwa pamoja bila kuwa katika kikao au darasa la pamoja tunaloonana ana kwa ana.

Msomi mmoja anaweza kuwa Uropa, mwingine Asia, mwingine Afrika na tukaweza kubadilishana mawazo muhimu kutokana na usomaji wetu. Ndiyo nguvu ya teknolojia tuliyo nayo. Tunao uwezo kwa kuwa tumejaliwa teknolojia. Sasa tufanye azimio na tujitahidi kulitekeleza kwa manufaa yetu wenyewe.

Mwandishi ni mhadhiri wa Lugha ya Kiswahili na Fasihi ya Kiafrika, Chuo Kikuu cha Mafunzo ya Kigeni cha Tianjin, Uchina.

[email protected]

You can share this post!

KAULI YA WALIBORA: Tukome kubeba dhana za Kiingereza...

PICHA: Nderemo nje ya mahakama baada ya Obado kuachiliwa

adminleo