• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
Raila aungwa mkono Rift Valley

Raila aungwa mkono Rift Valley

Na ONYANGO K’ONYANGO

WABUNGE kadhaa wa Rift Valley wamemtetea Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga baada ya wabunge wenzao kutoa wito kwake astaafu kwa sababu alipewa kazi katika Muungano wa Afrika (AU).

Wabunge hao walikosoa wenzao ambao wamekuwa wakimtaka Bw Odinga astaafu kutoka kwa siasa baada ya kuajiriwa kuwa Balozi Maalum wa Ustawishaji Miundomsingi barani Afrika wiki mbili zilizopita.

Mbunge wa Soy, Bw Caleb Kositany, alisema kiongozi huyo wa upinzani ana haki kuendelea kuwa katika siasa kwa sababu hakuna sheria inayomzuia kufanya hivyo.

“Bw Odinga hafai kustaafu kutoka katika siasa kwa sababu Katiba haijamzuia,” akasema Bw Kositany akiwa katika eneo la Kipsangui, Kaunti ya Uasin Gishu.

Alikashifu wabunge wanaozunguka nchini wakizungumzia siasa za urithi wa urais 2022 na kusema kuwa viongozi hivi sasa wanafaa wajishughulishe na masuala ya maendeleo na wakome kufanya kampeni za mapema.

Kulingana naye, Chama cha Jubilee kilifunga mjadala kuhusu urithi wa urais na sasa kinalenga kutekeleza ajenda nne kuu za maendeleo.

“Wanasiasa wanafaa wazikome siasa za 2022 na watekeleze ahadi zao walizotoa wakati wa kampeni. Ninataka kuambia wapinzani wetu kwamba katika Jubilee, tulimaliza siasa za 2022 kwa sababu William Ruto atakuwa mgombeaji wetu na kwa sasa tunashughulikia kumwezesha Rais Uhuru Kenyatta kuacha sifa bora,” akasema.

Aliongeza kuwa ifikapo 2022 itakuwa bora wagombeaji wote watie saini maelewano kwamba watakubali matokeo ya uchaguzi na kufanya kazi na yule atakayeshinda.

Mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter, alisema kuwa nchi bado yahitaji huduma za Bw Odinga kuendeleza uchumi wa taifa.

“Nchi hii bado inamhitaji Bw Odinga kuzungumzia ufisadi na kushirikiana kwa karibu na Rais ili kuwe na umoja. Raila anafaa tu kustaafu kutoka kwa siasa iwapo anahisi mwenyewe kwamba nchi iko salama na walio mamlakani wana uwezo wa kuielekeza inakofaa lakini kwa sasa bado kuna masuala mbalimbali ambayo waziri mkuu wa zamani anahitajika kutushauri kuyahusu,” akasema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Keiyo Kusini alisema itakuwa vyema kuwa na ushindani wa urais kati ya Bw Odinga na Naibu Rais ifikapo 2022.

“Siasa za Kenya hazitakuwa na mnato bila kuwepo kwa Bw Odinga na inafaa abaki katika siasa ndipo ulimwengu ushuhudie Bw Ruto atakavyomshinda. Viongozi wasionyeshe uoga kwa kumtaka astaafu,” akasema.

Wiki iliyopita, wabunge wandani wa Bw Ruto walizuru eneo la North Rift na kusema Bw Odinga anafaa kuondoka katika siasa ili ajishughulishe na majukumu yake mapya katika AU.

Wakiongozwa na Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro, walimtaka Bw Odinga aachie vijana siasa.

Naibu Kiongozi wa Ford Kenya, Dkt Boni Khalwale, aliunga mkono akisema Bw Odinga alianza siasa enzi za kina Rais Wastaafu Daniel arap Moi na Mwai Kibaki na hivyo basi ni vyema astaafu.

“Kama Bw Odinga akiutumia vyema wadhifa wake mpya, tutapata ufadhili zaidi kutoka kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa minajili ya kuboresha barabara zetu,” akasema Bw Khalwale.

Hata hivyo, wandani wa Bw Odinga wamekuwa wakisisitiza kuwa wadhifa wake mpya haumaanishi atastaafu kutoka siasa kwani wanamtarajia awanie urais tena ifikapo 2022.

You can share this post!

MAHINDI TELE, UGALI GHALI

Taharuki wanafunzi kutumiwa kadi ya rambirambi wakisubiri...

adminleo