• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
Gharama ya kuendesha magereza kupunguzwa

Gharama ya kuendesha magereza kupunguzwa

Na LUCAS BARASA

SERIKALI Jumatano inatarajiwa kutia saini mwafaka unaolenga kupunguza gharama ya kuendesha magereza ya humu nchini na kuziba mianya ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma.

Waziri wa Usalama Fred Matiang’i na mwenzake wa Huduma za Umma Margaret Kobia wanatarajiwa kutia saini mkataba wa maelewano ambao utawezesha Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) na Idara ya Magereza (KPS) kushirikiana katika utoaji wa huduma mbalimbali.

Mawaziri hao watatia saini mkataba huo katika Gereza la Kaloleni, Kaunti ya Kilifi.

“Maafikiano hayo yanalenga kuhakikisha kuwa shirika la NYS na idara ya KPS vinashirikina katika shughuli zitakazonufaisha taasisi zote mbili na kuziba mianya ya ufisadi,” ikasema taarifa ya serikali.

“Moja ya malengo makuu ya mwafaka huu ni kukomesha ufisadi katika utoaji wa kandarasi katika taasisi zote mbili. Mawaziri wote wawili wameafikiana kukomesha ufisadi ndani ya tasisi zilizo chini ya usimamizi wa wizara zao,” ikaongezea taarifa hiyo.

Dkt Matiang’i’s na Profesa Kobia pia watazindua kwa pamoja mradi wa uchimbaji wa kisima cha maji utakaotekelezwa na Magereza na shirika la NYS.

Wizara hizo mbili, kwa mfano, zitashirikiana katika uchimbaji wa visima na inakadiriwa kuwa hatua hiyo itasaidia kuokoa zaidi ya asilimia 50 ya fedha ikilinganishwa na kutoa kandarasi hiyo kwa kampuni za kibinafsi.

Shirika la NYS litajihusisha na uchimbaji wa visima vya idara ya magereza. NYS pia litashirikiana na magereza katika uzalishaji wa vifaa kama vile viti. Litajipatia vifaa vya samani kama vile viti kutoka kwa idara y a mahakama.

“Hili litasaidia kuokoa fedha kwani NYS watapata vifaa vya samani kwa bei ya chini ikilinganishwa na kununua vitu hivyo madukani,” ikasema taarifa.

Viti na vifaa vinginevyo vya samani kutoka idara ya mahakama hutengenezwa kwa ubora wa hali ya juu.

Kwa kununua viti vinavyotengenezwa na wafungwa, shirika la NYS litachangia pakubwa katika ufanikishaji wa kaulimbiu inayowataka Wakenya kununua bidhaa zinazotengenezwa na Wakenya humu nchini: ‘Nunua Kenya, Jenga Kenya’.

Shirika la NYS pia litapata vifaa vinavyotengenezwa kwa ngozi kama vile viatu kutoka idara ya magereza nchini.

Rais Uhuru Kenyatta hivi majuzi aliagiza viatu vinavyotumiwa na maafisa wa vikosi vya usalama kununuliwa humu nchini.

Shirika la NYS na idara ya KPS watashirikiana katika kampeni ya upanzi wa miti. Taasisi hizo mbili zinalenga kuhakikisha kuwa zinakuza miche 100 milioni kufikia Juni 2019.

Kuna jumla ya taasisi 129 za kurekebisha nchini Kenya.

Miongoni mwa taasisi hizo ni magereza 125, shule tatu za watoto wafungwa na kituo kimoja cha kutoa mafunzo na kurekebisha vijana.

You can share this post!

Kuwajali wakulima wa mahindi na miwa ni kukosa busara...

TAHARIRI: Wanaopachika watoto mimba wakabiliwe vikali

adminleo