• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
WANDERI: Waafrika wanachangia  ukoloni-mamboleo

WANDERI: Waafrika wanachangia ukoloni-mamboleo

Na WANDERI KAMAU

MIDAHALO ya ukombozi iliyoanzishwa na wanaharakati wa uhuru wa Mtu Mweusi katika miaka ya hamsini ilisisitiza kuhusu ‘kujipenda’ kwake kama nguzo kuu ya kujikomboa kutoka kwa minyororo wa wakoloni.

Midahalo hiyo iliendelezwa katika ulingo wa kisiasa, muziki na makongamano mbalimbali yaliyowashirikisha wanaharakati maarufu walioibukia kuheshimika katika harakati za ukombozi wa Weusi kote duniani.

Katika mojawapo ya hotuba zake kuhusu thamani ya Mtu Mweusi, rais wa kwanza wa Ghana, Kwameh Nkrumah alisema kuwa njia ya pekee ambapo angeweza kujikomboa ni kugundua thamani yake-kiundani na maumbile yake ya nje.

Hata hivyo, hili limeonekana kusahaulika na Waafrika wa kizazi cha sasa, kwani wanaendeleza ‘ukoloni-nafsi’ kwa kuwashabikia Wazungu wanaofika katika nchi zao kiasi cha kuwaabudu kama miungu wadogo.

Mifano halisi ni mwanahabari maarufu wa Shirika la CNN Richard Quest, mkewe rais wa Amerika Donald Trump, Melania Trump, aliyekuwa rais wa Amerika Barack Obama kati ya watu wengine “maarufu” kwa fasiri za sasa.

Alipowasili nchini mapema wiki iliyopita, Bw Quest alipokelewa katika hali ya “mshtuko” na baadhi ya watu. Katika “mshangao” huo, baadhi walinukuliwa wakisema kuwa hawangenawa mikono yao baada ya kumsalimia!

Zaidi ya hayo, Bw Quest alifanyiwa mahojiano mengi kuhusu mbinu za “uanahabari bora” kama kwamba wanahabari wa Kenya na Afrika kwa jumla hawana uelewa ama wamekuwa wakiendeleza shughuli zao kwa upofu wa kitaaluma.

Hali ilikuwa sawa kwa Bi Trump, ambapo hali iligeuka si hali alipowasili nchini. Maafisa wa usalama wa Kenya waliondolewa katika makazi aliyozuru, badala yake yakilindwa na vikosi maalum vya Amerika ili “kumhakikishia” usalama.

Na kama kejeli ya kiishara kwa Waafrika na “uhuru” wake, Bi Trump alivalia mavazi ya kikoloni, ambayo yalivaliwa na makaburu wa Kiingereza ambao waliwatesa na kuwadhulumu wapiganiaji wa vita vya ukombozi wa Kenya.

Alionekana kutotishika na lolote, ila lililomfurahisha ni “bashasha” ya Waafrika kung’ang’ania kupigwa picha naye, wakati akiwalisha Simba katika Mbuga ya Wanyamapori ya Nairobi.

Kwa wale wenye kumbukumbu nzuri, Bw Obama ‘hung’anganiwa’ kiwazi kila mara anapowasili nchini.

Wale ambao hufanikiwa kupigwa picha naye huzihifadhi kama kumbukumbu kwa wajukuu na vitukuu wao kuhusu walivyokutana na ‘mtu mkubwa’ duniani.

Kimsingi, kinachojitokeza wazi ni kwamba Waafrika wenyewe ndio hupanua jukwaa la Wazungu kuendeleza ukoloni-mamboleo dhidi yao.

Ung’ang’anizi huo wa kijinga ndio mwanamuziki Robert Nester Marley alioutaja kuwa jukwaa la “ukoloni-nafsi” au ukoloni wa kujitakia.

Mwandishi Ngugi wa Thiong’o huutaja kama “utumwa wa kiakili” kwenye maandishi yake mengi yanayokejeli mwigo wa tamaduni za Kizungu kama mojawapo ya sehemu za maisha ya Waafrika.

Sikatai kwamba Quest si mwanahabari maarufu, wala Obama ni mtu mwenye ushawishi. Hata hivyo, lazima tukumbuke kuwa wao ni binadamu kama sisi, ila hawana tofauti yoyote ya kimaumbile.

You can share this post!

TAHARIRI: Wanaopachika watoto mimba wakabiliwe vikali

Serikali ikate fungu la kumi kwenye mishahara ya waumini...

adminleo