• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:55 AM
Matokeo ya KCPE na uteuzi kwa Kidato cha Kwanza ni Novemba – KNEC

Matokeo ya KCPE na uteuzi kwa Kidato cha Kwanza ni Novemba – KNEC

Na PETER MBURU

KUFUATIA teknolojia ya usahihishaji wa kiautomatiki, Baraza la Kusimamia Mitihani Nchini (Knec) Jumatano limetangaza kuwa matokeo ya mtihani wa Kitaifa wa KCPE yatatolewa hapo Novemba.

Akizungumza katika shule ya msingi ya Uhuru Gardens Nairobi Jumatano, mwenyekiti wa Knec Profesa George Magoha alithibitisha kuwa kufikia mwisho wa Novemba matokeo yatakuwa tayari na uteuzi wa wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza kuanza mara moja.

“Tuna hakika kuwa matokeo yatakuwa tayari kufikia mwishoni mwa Novemba. Hii itafuatwa na uteuzi wa kujiunga na kidato cha kwanza kwa wanafunzi wanaofanya mtihani, jambo ambalo litawafanya wanafunzi kuripoti kidato cha kwanza awali mwaka ujao,” akasema Bw Magoha.

Bw Magoha alisema hivyo walipokuwa na Rais Uhuru Kenyatta, ambaye alifanya ziara ya ghafla kwa shule hiyo kuwahimiza watahiniwa na kuona namna shughuli ya mitihani inaendeshwa.

Rais Kenyatta alipiga gumzo na wanafunzi hao kwa dakika chache kabla yao kufanya mtihanoi wa Kiswahili.

“Kile mnachohitajika tu ni kutia bidi kabisa kadri mnavyoweza, mitihani ni kitu cha kupita tu. Kuna vitu vingine vingi maishani ambavyo mtahitajika kuvitoboa,” Rais Kenyatta akawaeleza wanafunzi.

Aliwahakikishia kuwa wote watapata nafasi ya kujiunga na shule za upili, huku waziri wa elimu Amina Mohamed ambaye aidha alikuwepo akihakikishia Rais kuwa mtihani wa mwaka huu unafanywa kwa njia bora zaidi kote nchini.

Jumla ya watahiniwa 1, 060, 703 wanafanya mtihani wa mwaka huu wa KCPE ambao unakamilika Alhamisi.

You can share this post!

Vyama 7 vya matatu vyapigwa marufuku na NTSA

Mama Jowie azirai kortini baada ya kilio mwanawe...

adminleo