• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Itumbi apamba mitandao kwa vilio baada ya Maribe kuzidi kuzuiliwa

Itumbi apamba mitandao kwa vilio baada ya Maribe kuzidi kuzuiliwa

Na PETER MBURU

MFANYAKAZI wa Ikulu Dennis Itumbi na ambaye pia alikuwa mpenziwe mwanahabari wa runinga ya Citizen anayekabiliwa na mashtaka ya Mauaji Jacque Maribe Jumatano alijaza vilio mitandaoni akidai kuwa kuna watu waliokuwa wakimzuia Bi Maribe kuachiliwa huru licha ya kulipa dhamana ya Sh1 milioni kama ilivyoamrisha korti.

Kupitia jumbe sita zilizoandamana katika mtandao wa Twitter, Bw Itumbi alidai kuwa naibu msajili wa mahakama za Milimani alikuwa akijivuta kuwakamilishia shughuli za kuwachiliwa kwa Bi Maribe, saa 24 baada yake kuruhusiwa kwenda nyumbani na korti.

Jumanne, Jaji James Wakiaga alimwachilia Bi Maribe huru kwa dhamana ya Sh1 milioni pesa taslimu, lakini akamzuilia rumande mshukiwa mwenza Joseph Irungu hadi Juni mwaka ujao kesi hiyo itakapoanza kusikizwa.

Hata hivyo, Bw Itumbi alilalamika kuwa kufikia saa nane Jumatano, Bi Maribe bado alikuwa katika gereza la wanawake la Lang’ata, kutokana na utepetevu wa baadhi ya maafisa.

Saa 8.31 alasiri, alituma ujumbe kupitia akaunti yake ya Twitter akisema “Matukio ya kufurahisha katika ofisi ya naibu msajili wa Mahakama Kuu. Tulimaliza mchakato wa bondi wa rafiki yetu Jacque Maribe saa sita adhuhuri na hadi sasa hakuna kinachoendelea na sasa anaelekea kulala usiku mwingine gerezani licha ya kuachiliwa na korti.”

Dakika tatu baadaye, alifuatisha ujumbe “Jana, michezo sawia ilichezwa. Naibu msajili alikataa kutia sahihi nakala kwa msajili wa ardhi na watu. Tuliamua kusubiri leo.

Dakika nne baadaye tena, Itumbi aliendelea “Asubuhi ya Jumatano familia na marafiki walifika Mahakama Kuu saa moja asubuhi na naibu Msajili akatia sahihi barua iliyokuwa katika dawati lake tangu jana jioni saa tano. Hatuna shida na hilo, tunaweza kuvumilia…”

Saa nane na dakika 44, afisa huyo wa ikulu aliendelea kuwa walielezwa kulikuwa na amri kuwa baada ya kuachiliwa kwa Bi Maribe, afisa anayechunguza kesi hiyo na wakili wake walifaa kukagua nyumba yake. Dakika moja baadaye alituma ujumbe mwingine kuwa viongozi wote wa mashtaka kutoka idara ya DPP walikata kutumiwa kufanya kazi hiyo.

“Hivyo tukaamua kutuma jumbe Twitter,” akasema.

Lakini vilio vya Itumbi mitandaoni vilionekana kuzaa matunda kwani dakika tatu baadaye alituma ujumbe mwingine akisema kuwa “Baada ya kutuma ujumbe wa kwanza Twitter, simu ambazo hazikuwa zikipokelewa na maafisa wa DCI na DPP sasa zimeanza kupigwa kwa haraka sana…asanteni sana.”

You can share this post!

DPP na EACC wazimwa kumshtaki Gavana Mutua kwa sakata ya...

Mwanamume mbioni kuhakikisha muafaka wa Uhuru na Raila...

adminleo