• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:54 PM
Mwanamume adai malipo kwa kaunti kwa kuinasia nyani 17

Mwanamume adai malipo kwa kaunti kwa kuinasia nyani 17

Na NDUNGU GACHANE

MWANAUME aliye na miaka 65 katika kijiji cha Githumu, kaunti ndogo ya Kandara, Kaunti ya Murang’a anataka serikali ya kaunti imlipe kwa kuwawinda nyani 17, kazi ambayo alipewa na kaunti hiyo.

Kamau Mungai alisimulia jinsi ujuzi wake wa kuwinda ulivyoishawishi serikali ya kaunti kuwapa mitego ya kuwanasa nyani baada ya kutangaza kazi hiyo na kuwataka walioitaka kutuma maombi kwenye ofisi za kaunti ndogo.

Aliongeza kwamba hata baada ya kuwapeleka nyani hao hadi kwa ofisi za kaunti, bado hajapata malipo yake na amekuwa akizungushwa na uongozi wa gavana Mwangi Wa Iria.

“Sina riziki kwa familia yangu. Naomba msaada wa wahisani ili kuishurutisha serikali ya kaunti inilipe. Juhudi zangu za kufikia gavana hazijafua dafu,” akasema Bw Mungai.

Akizungumza kwenye mkutano wa baraza katika kituo cha kibiashara cha Githumu uliohudhuriwa na mbunge wa Kandara Alice Wahome, Bw Mungai aliongeza kwamba yeye na mkewe waliteseka mno kuwajibikia kazi hiyo na akaamua kutorejesha mitego aliyokabidhiwa hadi apokee malipo yake.

Baada ya kukisikiza kilio chake, Bi Kandara alimlipa Sh100,000 alizodai kwa niaba ya gavana lakini cha kushangaza ni kwamba mwanaume huyo tena aliibua madai mapya akitaka alipwe riba ya Sh60,000.

“Ikiwa ningekopesha pesa basi ningelipa pesa zenyewe na riba. Hela nilizokabidhiwa na mbunge hazitoshi na nataka serikali ya kaunti ilipe zilizosalia,” akadai Bw Mungai.

Hata hivyo waziri wa kilimo wa kaunti Albert Mwaniki alitoa masharti yaliyomtaka Bw Mungai kurejesha mitego aliyopewa kwanza kabla ya mazungumzo yoyote kuandaliwa kuhusu malipo yake.

You can share this post!

Wateja wa Multichoice na DSTV kupata burudani zaidi Krismasi

Familia za walioangamia ajalini Kericho zadai fedha zao

adminleo