• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 2:56 PM
Sura 4 mpya Stars Migne akitarajia nyota wa majuu

Sura 4 mpya Stars Migne akitarajia nyota wa majuu

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Sebastien Migne, amekitaja kikosi cha wachezaji 30 atakachoanza kukitia makali wiki ijayo kwa minajili ya kibarua dhidi ya Sierra Leone katika jitihada za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019.

Wengi wa wachezaji ambao Migne amewaita kambini ni wale waliowategemea katika michuano miwili iliyopita ambayo iliwakutanisha Stars na Ethiopia jijini Bahir Dar na Nairobi mtawalia mnamo Oktoba 2018.

Sura mpya ambazo mkufunzi huyo mzawa wa Ufaransa amepania kujumuisha katika kikosi chake ni za kiungo Ayub Timbe ambaye amekamilisha marufuku ya michuano mitatu, Henry Ochieng, Jonah Ayunga na Masoud Juma. Ochieng na Ayunga wanavalia jezi za Braintree Town na Brighton mtawalia nchini Uingereza.

Kabla ya kuwaalika Sierra Leone jijini Nairobi Novemba 18 katika mechi ya marudiano ya Kundi F linalowajumuisha pia Ethiopia na Ghana, Kenya watashiriki mechi moja ya kirafiki kati ya Novemba 12 na Novemba 20, 2018.

Iwapo wataibuka miongoni mwa timu mbili za kwanza katika Kundi F, Stars watapiga kambi nchini Ufaransa kwa kipindi cha majuma mawili ya kujifua kabla ya kuelekea Cameroon kwa fainali za AFCON 2019.

Haya ni kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa.

Kufikia sasa, wako pazuri zaidi kushiriki mapambano hayo ya AFCON kwa mara ya kwanza tangu 2004 baada ya kujizolea alama saba kutokana na mechi nne zilizopita dhidi ya Sierra Leone, Ghana na Ethiopia.

Kenya walifungua kampeni zao za Kundi F kwa kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Sierra Leone jijini Freetown mnamo Juni 2017 kisha kuwapepeta Ghana 1-0 katika mchuano uliowakutanisha jijini Nairobi mnamo Septemba 8, 2018.

Vijana hao wa Migne waliambulia sare tasa dhidi ya Ethiopia katika mchuano wa mkondo wa kwanza ugenini kisha kuwapepeta 3-0 katika marudiano yaliyoandaliwa uwanjani MISC Kasarani mnamo Oktoba 14, 2018.

Kenya walinogesha fainali za AFCON kwa mara ya mwisho miaka 14 iliyopita waliposhiriki kindumbwendumbwe hicho nchini Tunisia.

KIKOSI CHA STARS:

MAKIPA: Patrick Matasi (St Georges, Ethiopia), Farouk Shikalo (Bandari), Brian Bwire (Kariobangi Sharks).

MABEKI: Musa Mohammed (Nkana FC, Zambia), Brian Mandela (Maritzburg United, Afrika Kusini), David Ochieng (IF Brommapojkarna, Uswidi), Abud Omar (Cercle Brugge, Ubelgiji), Erick Ouma (Vasalund, Uswidi), Joseph Okumu (Real Monarchs, Amerika), Philemon Otieno (Gor Mahia), Bernard Ochieng (Vihiga United), Joash Onyango (Gor Mahia),

VIUNGO: Ismael Gonzalez (Las Palmas, Uhispania), Victor Wanyama (Tottenham Hotspur, Uingereza), Anthony Akumu (Zesco United, Zambia), Ayub Timbe (Beijing Renhe, China), Johanna Omollo (Cercle Brugge, Ubelgiji), Eric Johanna (IF Brommapojkarna, Uswidi), Paul Were (FC Kaisar, Kazakhstan), Henry Ochieng (Braintree Town, Uingereza), Francis Kahata (Gor Mahia), Hassan Abdallah (Bandari), Cliff Nyakeya (Mathare United), Dennis Odhiambo (Sofapaka).

WAVAMIZI: Michael Olunga (Kashiwa Reysol, Japan), Jonah Ayunga (Sutton United, Uingereza), Masud Juma (Aj Fujairah, UAE), Ovella Ochieng (Vasalund, Uswidi), Allan Wanga (Kakamega Homeboyz), Piston Mutamba (Sofapaka).

You can share this post!

KWA KINA: Jowie alipiga na kupokea simu zaidi ya mara 100...

UBINGWA EPL: Kazi bado ipo

adminleo