• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
MOHAMMED: Twastahili kukataa njama za China kutudhibiti kiuchumi

MOHAMMED: Twastahili kukataa njama za China kutudhibiti kiuchumi

Na MAINA MOHAMMED

WINGU jeusi la kibiashara linatishia mahusiano kati ya Kenya na China. Haya ni baada ya Kenya kuweka vikwazo vya kibiashara katika uagizaji wa samaki kutoka China. Kenya imechukua hatua hii ili kulinda wavuvi na pia walaji samaki.

China kupitia kaimu balozi wake humu nchini Li Xuhang imetishia kujibu ‘kipigo’ hiki. Kulingana na wachanganuzi wa masuala ya kiuchumi miradi ambayo inaweza kuathirika ni ile ya ujenzi wa miundombinu inayofadhiliwa na China.

Hapa maendelezo ya ujenzi wa ule mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Naivasha kwenda Kisumu unaweza kuwa mhanga wa kwanza. Kubana pesa za mradi huu ni silaha ambayo China?inaweza kutumia ili kuifanya serikali ya Kenya kusalimu amri.?Lakini kwangu mzozo huu ni fursa kwa Kenya kutathimini mahusiano yake na China. Mahusiano haya katika nyanja ya kibiashara yamekuwa na dhuluma dhidi ya Kenya.

Kati ya mwezi Januari na Mei 2018 tofauti thamani ya biashara kati ya nchi hizi ilikuwa Ksh 494.26 bilioni. Hii ina maana kuwa wakati China iliuzia Kenya bidhaa za thamani ya Sh494.26 bilioni, Kenya haikuuzia China chochote.

Uhusiano wa aina hii wa kibiashara una matokeo ya kuua viwanda vyetu na kupunguza ajira.?Ni uhusiano unaoongezea umaskini Kenya na kuongeza utajiri China. Ama kama taifa lazima kusimame pamoja kulinda maslahi yetu. Hatuwezi kuruhusu China kutugeuza kuwa soko huria la bidhaa na?huduma zake.

Hali ya Wachina kutwaa hata biashara za uchuuzi kwenye mitaa ya miji yetu ni kichocheo cha umaskini wetu wa kipato. Hapa lazima bunge letu litunge upya sheria za kazi zinazoruhusu wageni kuishi na kufanya biashara hapa Kenya.

Kwa hali zote lazima sheria zetu zilinde sekta ya Jua Kali bila kujali dhana ya masoko huria na utandawazi. Kufungua masoko yetu kwa kila aina ya bidhaa zikiwemo zile bandia ni sawa na kujitia kitanzi wenyewe. Taasisi zinazohusika na kuhakikisha ubora wa bidhaa lazima zibane kuingizwa kwa bidhaa duni na hatari kutoka China.

Aidha katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ni muhimu kuweka mipaka na viwango. Wachina wasiruhusiwe kuagiza wafanyakazi kwa ‘shughuli za mikono’ kama vile kukoroga zege au shughuli zingine zinazoweza kutekelezwa na Wakenya.

Kwamba mikopo yao ndiyo inayoendesha miradi hii isiwe sababu yao kudhibiti uchumi wetu huku wakijiita washirika wetu wa maendeleo. Mizungu ya kidiplomasia ya mikopo na ufadhili isiwe silaha kutugeuza kuwa tegemezi kwa China.?Uhusiano wetu na China uongozwe na maslahi yetu sio yale ya China.

You can share this post!

TAHARIRI: Walioagiza mahindi mabovu waanikwe

Bolt ang’atuka baada ya klabu kudinda kumpa mamilioni...

adminleo