• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
KUTULIZA JOTO: Uhuru ampeleka Raila kwa Ruto

KUTULIZA JOTO: Uhuru ampeleka Raila kwa Ruto

CHARLES WASONGA na IBRAHIM ORUKO

SIKU moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kudai kuwa atawashtua Wakenya kuhusu atakayempendekeza kuwa mrithi wake 2022, Naibu Rais William Ruto Ijumaa aliwashangaza wengi kwa kumwalika rais nyumbani kwake Karen, Nairobi, kwa chakula cha mchana.

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, ambaye ni hasimu wa Ruto kisiasa, pia alialikwa kushiriki chakula hicho. Kiongozi huyo wa ODM aliwasili katika makazi hayo rasmi ya Naibu Rais, akiandamana na mfanyabiashara Jimmi Wanjigi, dakika 20 baada ya Rais kuwasili.

Japo maelezo kamili kuhusu yaliyojadiliwa katika mkutano huo hayakutolewa rasmi inaaminika kuwa watatu hao walijadili masuala mengi yanayohusu taifa hili, zikiwemo siasa.

Duru zilidokezea Taifa Leo kuwa, Ruto alimwalika Rais Kenyatta pekee katika maankuli hayo lakini rais akaamua ‘kumvuta’ Bw Odinga ili waandamane pamoja.

“Tulijadili masuala yanayohusiana maendeleo ya kitaifa na umoja,” Bw Ruto akasema kupitia ujumbe kwenye ukurasa wake wa twitter. Haikubainika iwapo mkutano huo ulipangwa au ulikuwa ni sadifa tu.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bw Ruto kuwaketi pamoja na Rais Kenyatta na Bw Odinga tangu wawili hao walipozika tofauti zao za kisiasa kwa kutia saini muafaka wa maelewano mnamo Machi 9 mwaka huu.

Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen aliungana na watatu hao katika mazungumzo yaliyodumu saa moja. Alidinda kutoa maelezo kuhusu yaliyojadiliwa katika mkutano huo akisema: Naibu Rais alitaka kuonyesha kuwa yeye pia anakumbatia moyo wa maridhiano na kuonyesha kuwa yu tayari kufanyakazi na Bw Odinga katika kipindi hiki cha maridhiano. Ni hayo tu, hakuna mengine,” Bw Murkomen akasema.

Awali, viongozi hao walikuwa wamehudhuria ibada ya wafu ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake (MYWO) marehemu Jane Kiano katika Kanisa la Kianglikana la St Francis, Karen.

Mnamo Alhamisi Rais Kenyatta aliwashangaza Wakenya aliposema kuwa atakuwa na usemi katika siasa za urithi wa kiti chake atakapostaafu mnamo 2022.

“Watu wengine wanadhani kwamba kwa sababu ninastaafu sina cha kusema katika siasa za urithi zinazoendelea. Nitakuwa na la kusema wakati ukifika na watu wengine watashangazwa na chaguo langu,” akasema alipoongoza halfa ya ufunguzi wa soko kubwa la Karatina, kaunti ya Nyeri.

Rais Kenyatta aliwakaripia wanasiasa ambao wameanza siasa za mapema za uchaguzi mkuu wa 2022, akisema huu ni wakati wa maendeleo sio kuchapa siasa.

Kulingana na makubaliano kati ya Rais Kenyatta na Ruto mnamo 2012, baada ya Rais kustaafu, chama cha Jubilee kitamuunga naibu wake kwa kiti cha urais.

Baadhi ya wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya, ambalo ni ngome ya kisiasa ya Bw Kenyatta, wamekuwa wakimpigia debe Bw Ruto kupitia vuguvugu linalojulika kama “Team Tangatanga”.

Wiki moja iliyopita Rais Kenyatta aliripotiwa kuwaambia wafuasi wa Jubilee katika eneo la Rift Valley, ambalo ni ngome ya kisiasa ya Bw Ruto, kwamba makubaliano yao yangalipo.

Badala yake alilaumu vyombo vya habari kwa kueneza uvumi kwa kueneza uvumi kuhusu kuwepo kwa mgawanyiko katika chama cha Jubilee kuhusu siasa za urithi.

Lakini mamo Alhamisi, akiongea katika ngome yake ya Mlima Kenya, Rais Kenyatta alionekana kubadili msimamo tena akisema “ni mapema kuangazia siasa kampeni za 2022.”

“Watu wengine wanatumia muda wao mwingi kuongeza kuhusu mambo ya kesho, lakini hawajafanya lolote leo. Watu wanafaa kukoma kuchapa siasa na wafanye kazi.” akasema kabla ya kufanya mkutano na viongozi wa eneo la Kati mwa Kenya katika Makao Makuu ya Kamishna wa Kaunti ya Nyeri.

Hatua ya Bw Odinga kufika nyumbani kwa Ruto iliwashangaza wengi ikizingatia kuwa wawili hao ni mahasidi wa kisiasa. Mwezi jana Naibu Rais alimshambulia Bw Odinga kwa madai kuwa alikuwa akipanga njama ya kumfurusha (Ruto) kutoka chama tawala cha Jubilee.

You can share this post!

Mkurugenzi aliyetimuliwa aitaka National Bank imlipe Sh450...

Mzee Moi amuita Kalonzo kwa mazungumzo

adminleo