• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Ruto kuzuru ngome ya Obado

Ruto kuzuru ngome ya Obado

Na ELISHA OTIENO

NAIBU wa Rais William Ruto anatarajiwa kuzuri kaunti ya Migori Jumatatu kuzindua mradi wa ujenzi wa barabara, ikiwa mara ya kwanza kwake kuzuru eneo hilo ngome ya ODM, tangu miaka miwili iliyopita alipofika eneo la Nyatike kuzindua mradi wa stima.

Bw Ruto ambaye atakuwa kaunti ndogo ya Suna West vilevile atahutubia umma, katika hafla ambayo mwenyeji wake atakuwa Gavana wa Migori Okoth Obado.

Naibu wa Rais anatarajiwa kuzindua ujenzi wa barabara ya kutoka Masara hadi Muhuru beach, huku mkurugenzi wa mawasiliano katika ofisi ya gavana Nicholas Anyuor akisema maandalizi kwa ajili ya ziara yake inaendelea.

“Tuko tayari kabisa kumpokea naibu wa Rais Jumatatu kwa ziara hiyo ya maendeleo,” Bw Anyuor akasema.

Ujenzi wa barabara hiyo ya kiwango cha juu ulikuwa umekwama katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Lakini ziara hiyo ya Bw Ruto inatarajiwa kuvuta tafsiri za kisiasa, haswa ikija muda mfupi baada ya Bw Obado kutengana na uongozi wa ODM kuhusiana na uteuzi wa Bw Ochillo Ayacko katika uchaguzi mdogo wa useneti kaunti ya Migori siku chache zilizopita.

Gavana huyo alikosoa hatua ya chama na kumuunga mkono mwaniaji wa chama cha FPK Eddy Oketch, ambaye baadaye alipoteza kwa Bw Ayacko.

Ziara hiyo vilevile inakuja siku chache baada ya gavana huo kuachiliwa kutoka jela ya Industrial Area, Nairobi ambapo alikaa kwa zaidi ya mwezi kuhusiana na mashtaka anayokumbana nayo ya mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Sharon Otieno.

Kwa sasa, Bw Obado yuko nje kwa dhamana ya Sh5 milioni, pamoja na masharti mengine makali aliyopewa na korti, ambayo yamemzuia kusafiri kwa njia huru popote atakapo.

Hali kuwa Bw Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wamekuwa na uhusiano mbaya wa kisiasa aidha inatarajiwa kuchochea cheche za maneno kutoka kwa viongozi wa eneo hilo.

Katika ziara zake za mbeleni kaunti hiyo, Bw Ruto amekuwa akitembelea maeneo ya Kuria Mashariki na Magharibi ambapo chama chake cha Jubilee kina uungwaji mkono mkubwa, lakini wakati huu kwa mara ya kwanza ameamua kwenda hadi mlangoni mwa ngome ya ODM.

Viongozi wawili kutoka kaunti hiyo eneo la Kuri ni wa chama cha Jubilee, Bw Matthias Robi akiwa Kuria Magharibi na Kitayama Maisori wa Kuria Mashariki.

You can share this post!

Serikali sasa kufuatilia mawasiliano ya WhatsApp

Madereva wasimulia kukutana na jini jike

adminleo