• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
MURKOMEN: Tutamnasa Raila amuunge mkono Ruto 2022

MURKOMEN: Tutamnasa Raila amuunge mkono Ruto 2022

IRENE MUGO Na VALENTINE OBARA

MRENGO wa Naibu Rais William Ruto umefichua kuwa unajaribu kumshawishi kiongozi wa ODM Raila Odinga kumuunga mkono kuwania urais 2022.

Kulingana na mwandani wa Bw Ruto, Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet, hii ni moja ya mbinu ambazo Naibu Rais anatumia kuafikia lengo lake la kuwa rais wa Kenya.

Mbinu nyingine ambayo Naibu Rais ametilia mkazo ni ziara nyingi katika maeneo mahsusi hasa Pwani, Magharibi na Kati, ambapo amekuwa akishawishi wanasiasa kumuunga mkono katika azma yake na kufanya hivyo kwa kutangaza hadharani.

Tayari amepenya ngome ambazo awali zilikuwa za Bw Odinga na kufanikiwa kupata wabunge na viongozi wengine kujitokeza na kumhakikishia kuwa wako nyuma yake katika safari ya 2022.

Akiongea katika Kaunti ya Nyeri, Bw Murkomen alisema Bw Odinga akinyemelewa kwa uangalifu anaweza kukubali kumuunga mkono Bw Ruto.

Mnamo Ijumaa, Bw Murkomen aliungana na Bw Ruto, Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta nyumbani kwa Naibu Rais kwenye kikao ambacho yaliyojadiliwa hayakufichuliwa.

“Ndio sababu ninawaambia wabunge tusisumbue huyu mzee kwani amekuwa mtu mkubwa. Uhuru ameleta yeye karibu… Niliona juzi Naibu Rais ameita lunch na wakaketi pamoja. Mimi nilikuwa kwa kona kama ‘observer’. Lakini vile ‘niliobserve’, Raila anaweza akasaidia Ruto akuwe rais,” akasema Bw Murkomen.

Seneta huyo aliwaambia wabunge wa Jubilee waache kumshambulia Bw Odinga na badala yake waunge mkono mwafaka wake na Rais Kenyatta.

Matamshi hayo yanaonyesha mabadiliko ya msimamo wa Bw Murkomen, ambaye awali hakuonekana kuchangamkia Bw Odinga kuwa karibu na Rais Kenyatta.

Hayo yanajiri huku kwa upande wake Bw Odinga akionekana naye anajipanga kuhusu 2022. Hapo jana alisafiri kuelekea Uingereza akiwa pamoja na Mbunge wa zamani wa Gatanga, Bw Peter Kenneth.

Ingawa ilisemekana wameenda kutazama mechi ya kandanda kati ya timu za Gor Mahia na Everton ya Uingereza itakayochezwa leo, ziara hiyo imetokea wakati ambapo wanasiasa wanaomezea mate kiti cha urais 2022 wanazidi kujipangia mikakati.

Wadadisi wa siasa humtaja Bw Kenneth kama mmoja wa viongozi wa Mlima Kenya ambao huenda wanaandaliwa kumrithi Rais Kenyatta kama kigogo wa kisiasa eneo hilo wakati Rais Kenyatta akistaafu.

Baadhi ya viongozi wa eneo hilo humshinikiza rais atoe mwelekeo kuhusu hali ya kisiasa itakavyokuwa kwa jamii yao atakapostaafu, ingawa yeye hupuuzilia mbali suala hilo.

Wiki iliyopita baada ya kukutana na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya katika Kaunti ya Nyeri, rais alisema uamuzi atakaofanya kuhusu siasa za 2022 utashtua wengi.

Mnamo Septemba, Bw Odinga alikutana na Bw Kenneth afisini mwake katika jengo la Capitol Hill jijini Nairobi na kuibua mijadala kwenye ulingo wa kisiasa kwamba huenda wawili hao wanapanga kushirikiana 2022.

Baada ya mkutano wao wakati huo, waziri huyo mkuu wa zamani alimsifu Bw Kenneth kama mtaalamu shupavu wa masuala ya usimamizi wa uchumi wa taifa na kwamba walijadiliana kuhusu uchumi na mwafaka kati yake na Rais Kenyatta unaolenga kukabiliana na siasa za kikabila zinazosababisha migawanyiko nchini kila wakati wa Uchaguzi Mkuu.

“Peter Kenneth ni rafiki yangu na tulifanya kazi naye kwa karibu wakati wa serikali ya mseto alipokuwa waziri msaidizi wa fedha. Nimemwarifu pia kuhusu handsheki na malengo yake kuleta umoja ili tuangamize ukabila na tupige kasi maendeleo ya wananchi wetu,” alisema.

Kwa upande wake Bw Kenneth alisifu lengo la mwafaka wa Bw Odinga na Rais Kenyatta kuleta umoja nchini.

You can share this post!

KCSE: Mtahiniwa aaga mara baada ya kumaliza mtihani wa...

KCSE: Ajabu ya wasichana 13,600 kupata mimba Kilifi

adminleo