• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KCSE: Watahiniwa 200 wahepa mtihani, wasichana zaidi wajifungua

KCSE: Watahiniwa 200 wahepa mtihani, wasichana zaidi wajifungua

Na WAANDISHI WETU

MAMIA ya wanafunzi wa kidato cha nne wamehepa kufanya mtihani wa kitaifa unaoendelea wa KCSE.

Katika eneo la Pwani, zaidi ya wanafunzi 200 waliokuwa wamesajiliwa kufanya mtihani huo mwaka huu walitoweka bila sababu mahsusi.

Sababu zilizotolewa na wazazi ni kuwa baadhi wamesafiri, wengine wamejiunga na makundi ya ujambazi ama kuolewa na wengine wamesafiri nje ya nchi.

Maafisa wa usalama wamekuwa wakifuatilia visa vya wanafunzi wa hata miaka 11 Mombasa kujiunga na makundi ya uhalifu ya ‘Wakali Kwanza’, ‘Wakali Wao’ na ‘Wajukuu wa Bibi’, na inashukiwa walikataa kwenda kufanya mtihani wakihofia kukamatwa ama hawakuwa wamejitayarisha.

Katika Kaunti ya Mombasa watahiniwa 70 walikosa mtihani huo huku kaunti zingine zikiwa Kwale 19, Kilifi 55, Tana River 10, Taita Taveta 24 na Lamu 6.

Katika Kaunti ya Kisii, watu 16 wakiwemo walimu walishtakiwa kwa udanganyifu na wakawekwa rumande kwa siku tano ili polisi wakamilishe uchunguzi wao.

Katika Kaunti ya Taita Taveta, mtahiniwa wa Shule ya Upili ya Marugu alipoteza uwezo wa kuona ghafla alipokuwa akifanya mtihani wa Kiingereza jana. Alipelekwa hospitalini baada ya kushindwa kufanya mtihani.

Nao watahiniwa 11 kati ya 82 ambao walisajiliwa kama watu wazima walihepa mtihani huo katika Kaunti ya Kisii.

Mkurugenzi wa elimu ya watu wazima eneo hilo George Orwa, alisema kuwa baadhi ya watahiniwa wengine walipeana sababu zao za kukosa kufanya mtihani huo, huku wengine wakihepa licha ya kuhudhuria matayarisho Ijumaa wiki jana.

Katika Kaunti ya Kitui, watahiniwa 72 wana mimba na wengine 38 walijifungua usiku wa kumkia mtihani Jumatatu.

Kulingana na Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Kitui, Bw Salesa Adano, idadi hiyo ni kubwa sana na huenda ikawa zaidi.

Kulingana na mkurugenzi huyo, mipango imefanywa kwa lengo la kuhakikisha kuwa watahiniwa wote wamefanya mtihani hata walio hospitalini.

Mtahiniwa mmoja aliahirisha mtihani hadi mwaka ujao baada ya kupatwa na uchungu wa kujifungua. Mwanafunzi huyo wa Shule ya Upili ya Precious Blood, Tyaa iliyoko Mwingi, alikimbizwa katika Hospitali ya Mwingi Leval Four alikofanyiwa upasuaji baada ya kupata matatizo wakati wa kujifungua.

Kulingana na afisa wa elimu Mwingi ya Kati, Bw Joseph Javi, mwanafunzi huyo aliandika barua kwa Wizara ya Elimu kuahirisha kufanya mtihani kutokana na upasuaji huo.

Mwanafunzi mwingine wa Shule ya Upili ya Enziu alipatwa na uchungu wa kujifungua alipokuwa akikalia mtihani wa Kiingereza na akakimbizwa katika Hospitali ya Mumbuni alikojifungua na kuendelea na mtihani wake hospitalini humo.

Jumatatu, watahiniwa wanne walijifungua katika Hospitali ya Mwingi Level Four na Kitui Level Five. Watahiniwa hao walikuwa wa kutoka shule za IPC Mathuma, Enzuva, Vinda na Shule ya Upili ya Ungatu.

Katika Kaunti ya Machakos, mtahiniwa katika Shule ya Upili ya Makiliva alifanyia mtihani wake katika Hospitali ya Mwala Level Four baada ya kujifungua Jumatatu.

Mkurugenzi Mkuu wa TSC katika Kaunti ya Machakos David Mukui alisema mtahiniwa huyo na miaka 17 alikimbizwa hospitalini baada ya kuanza kuumwa akifanya mtihani Jumatatu.

Katika Kaunti ya Isiolo, watahiniwa saba walianza mtihani wao wakiwa wajawazito, watano kati yao tayari wamejifungua kulingana na afisa mmoja wa elimu eneo hilo.

Watahiniwa wawili nao kutoka Kaunti ya Kisii wanaendelea kufanya mtihani katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt Enock Ondari, mmoja wa watahiniwa hao alihamishwa kutoka zahanati ndogo akiwa na matatizo na baadaye kajifungua mtoto kabla ya wakati wa kuzaa kufika.

Dkt Ondari alieleza kuwa mtahiniwa mwingine alijifungua kawaida na yuko tayari kuruhusiwa kwenda nyumbani ili aendele na mtihani.

Naye mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Mororo, Kaunti ya Tana River, anakalia mtihani wake katika jela ya King’ong’o, Kaunti ya Nyeri.

Mwanafunzi mwingine wa Shule ya Sekondari ya Madogo Muslim hatafanya mtihani baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani na amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Garissa.

Mtahiniwa mwingine wa Shule ya Sekondari Hirimani, Kaunti Ndogo ya Bura alitoroka siku ya kufanya majaribio.

Wakati huo huo, wasimamizi wa shule wameagizwa wawe wakitoa takwimu za kila mwezi za wanafunzi wajawazito shuleni mwao.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dkt Belio Kipsang, walimu wanaokataa kutoa takwimu hizo watachukuliwa hatua za kinidhamu.

You can share this post!

MUGO WA WAIRIMU: Daktari kutoka kuzimu

EACC yaagizwa kumrudishia Kidero mali yake ndani ya saa 72

adminleo