• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
Tunakungoja 2022, wakulima wamwambia Ruto

Tunakungoja 2022, wakulima wamwambia Ruto

BARNABAS BII na CHARLES WASONGA

WAKULIMA wa mahindi kutoka eneo la Rift Valley wamelalamikia kimya cha Naibu Rais William Ruto na wanasiasa kutoka eneo hilo kufuatia hatua ya serikali kupunguza bei ya kununua zao hilo msimu huu kutoka Sh3,200 hadi Sh2,300.

Wameapa kuwaangusha wabunge, maseneta na magavana, ambao wamefeli kutetea masilahi yao, katika uchaguzi mkuu wa 2022.

“Ni jambo lisilotarajiwa kwa Naibu Rais kuendelea kunyamazia masuala ambayo yanaathiri ngome yake ya kisiasa,” akasema David Too ambaye ni mkulima kutoka eneo la Moiben, kaunti ya Uasin Gishu.

Alimtaka Bw Ruto kutangaza msimamo wake kuhusu bei mpya ya mahindi.

Naye mkulima Jackson Kosgey kutoka Saos, kaunti ya Nandi alisema wataendesha kampeni dhidi ya wabunge, maseneta na magavana ambao wamefeli kuangazia masaibu yao.

“Tumekuwa tukifuatilia utendakazi wa viongozi wetu tuliowachagua, haswa kuhusu masuala ya kilimo. Tutawaangusha wale ambao wamajitia hamnazo kuhusu masaibu yetu,” akasema.

Mnamo Jumatatu, Bodi ya Hazina ya Uhifadhi wa Chakula Nchini (SFRTF) ilipunguza bei ya mahindi kutoka Sh3,200 hadi Sh2,300 katika msimu huu wa mavuno.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dkt Noah Wekesa alitetea bei hiyo akisema imekadiriwa kwa kuzingatia gharama ya uzalishaji wa mahindi na hali kwamba mwaka huu wakulima wa humu nchini na mataifa jirani walipata mavuno mazuri ikilinganishwa na mwaka jana.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Wakulima Nchini (KFA) Kipkorir Arap Menjo aliikosoa serikali kwa kushindwa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu gharama ya uzalishaji mahindi kwa kuwahoji wakulima wenyewe.

“Kuanzishwa kwa ushuru wa ziada ya thamani wa (VAT) wa kima cha asilimia 8 kwa bidhaa za mafuta kumechangia kupanda kwa gharama ya uzalishaji kwa kiwango cha asilimia 15,” akasema.

Na jana, Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, alijipata katika hali ngumu alipofika mbele ya wabunge kuangazia suala hilo, kati ya masuala mengine yanayohusu wizara yake.

Waziri aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo kwamba, bei hiyo ya Sh2,300 ilifikiwa baada ya maafisa wa wizara yake kuzingatia gharama ya uzalishaji mahindi, kati ya masuala mengine yanayohusu zao hilo.

“Bei hii ilifikiwa baada ya maafisa wa bodi ya SFRTF kuendesha ukadiriaji wa gharama ya uzalishaji mahindi ambayo ilipatikana kuwa Sh1,530 kwa gunia moja la kilo mia moja. Kwa hivyo, baada ya kuongezewa gharama zingine za ziada, ndipo bei ya Sh2,300 ikafikiwa,” Bw Kiunjuri akawaambia wabunge hao.

Hata hivyo, wabunge Silas Tiren (Mioben), Ferdinand Wanyonyi (Kwanza) na Emmanuel Wangwe (Navakholo) walipuuzilia mbali bei hiyo wakimtaka Bw Kiunjuri kuwasilisha mwongozo wa namna ilivyokadiriwa.

“Bei hii ni duni zaidi na wakulima wa mahindi hawataikubali ikizingatiwa kuwa gharama ya uzalishaji wa mahindi iko juu. Hii ni kufuatia hatua ya serikali kuanzisha ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kwa mafuta na kemikali za kuangamiza wadudu,” akalalama Bw Tiren ambaye pia ni mkulima mashuhuri eneo la Uasin Gishu.

You can share this post!

Waziri alaumiwa kwa mimba za wanafunzi

RUTO ARUDI NYANZA TENA

adminleo