• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Uhuru na Ruto wanatisha watahiniwa wa KCSE – KUPPET

Uhuru na Ruto wanatisha watahiniwa wa KCSE – KUPPET

Na TOM MATOKE

CHAMA cha Walimu wa Upili (KUPPET) kimewaomba Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na mawaziri kukoma kwenda katika shule wakati wa mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) unaoendelea.

Mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Akelo Misori, alisema jana kuwa badala yake, serikali inapaswa kuweka juhudi zake katika kukabili ufisadi. Alisema kuwa uwepo wao shuleni unawatia hofu wanafunzi.

“Uwepo wa Rais, naibu wake na mawaziri haufaidi watahiniwa kwa vyovyote vile, ila unawatia hofu. Tumebaini kwamba wanafunzi wanajawa na hofu kwa hadi dakika 30 kila wakati maafisa wakuu wa serikali wanapozuru shule zao wakati wa mitihani,” akasema Bw Misori.

Akaongeza: “Rais Kenyatta na Bw Ruto ndio watakuwa wa kulaumiwa ikiwa wanafunzi wataanguka mitihani hiyo. Serikali imeifanya mitihani hiyo kuwa kama opereheni ya usalama.”

Mwenyekiti huyo alikuwa akihutubu katika mkutano wa walimu katika Kaunti ya Nandi.

Naibu Mwenyekiti wa chama hicho Julius Korir alisema ingawa hawaungi mkono udanganyifu katika mitihani, haifai viongozi wa kisiasa kuendelea kutembelea shule wakati wa mitihani.

“Uongozi wa serikali umeshindwa kukabili ufisadi. Hatuwataki kuzuru shule za upili. Kwa namna fulani, wanaathiri mitihani hiyo kwa kujiongezea marupurupu ya mamilioni ya fedha bila kumjali mlipa ushuru,” akasema Bw Korir.

“Wanaandamana na walinzi na wasaidizi wa kibinafsi wanaotumia fedha nyingi. Serikali haifanyi juhudi zozote kupunguza kiwango cha pesa zinazotumika katika mambo yasiyo muhimu. Wananchi wanaumia,” akasema Bw Korir.

Wakati huo huo, chama kililiomba Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) kuhakikisha kuwa sheria zote za mitihani zimezingatiwa na kila mmoja, hata iwe ni rais.

You can share this post!

Maswali yaibuka kuhusu kimya cha ziara za rais

Akasha waugua wakiwa gerezani jijini New York

adminleo